Utangulizi
Barua hii iliandikwa na Paulo katika siku za mwisho za maisha yake, na alimwandikia mwenzake katika huduma Timotheo, ambaye alikuwa amemwacha Efeso ili arekebishe baadhi ya shida zilizokuwemo kanisani. Kufikia wakati huu shida zinazohusu mafunzo, tabia kanisani, uongozi wa kanisa, na mambo kadhaa ya kuishi kama Mkristo yalikuwa yamejitokeza. Paulo aliandika kumwagiza Timotheo kuhusu mambo haya ili kanisa liweze kuendelea vyema. Pia aliandika na nia ya kumtia moyo Timotheo ili asife moyo katika maisha yake ya Ukristo, bali aishi maisha matakatifu ya kumtukuza Mwenyezi Mungu. Kuna kanuni maalum inayotolewa kwa wanaotaka kusimikwa kama viongozi wa kanisa pia.
Wazo Kuu
Umuhimu wa imani sahihi na tabia njema ndiyo kiini cha kitabu hiki. Paulo anatilia mkazo kwamba lazima tujue ukweli na kuutetea dhidi ya mafunzo ya uongo yanayoinuka. Lazima pia tuwe waangalifu kabisa katika kuishi maisha yanayoambatana na mafunzo hayo, ili Shetani asipate fursa ya kuwadanganya watu wa Mwenyezi Mungu. Umuhimu wa watu waliojitoa na walio watakatifu katika kuliongoza kanisa pia umekaziwa.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Hapajulikani.
Tarehe
Kama mwaka wa 64 B.K.
Mgawanyo
• Maonyo kuhusu mafundisho ya uongo (1:1-20)
• Maagizo kuhusu maombi (2:1-15)
• Kuhusu kusimikwa kwa maaskofu na mashemasi (3:1-16)
• Himizo na huduma (4:1–5:25)
• Huduma ya Ukristo, na maagizo kwa Timotheo (6:1-21).