Utangulizi
Kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati kinaendelea kuzungumzia historia ya Yuda iliyoanza katika 1 Mambo ya Nyakati. Kinahusu utukufu wa utawala wa Sulemani, mkazo ukitiliwa kwa utukufu wa Hekalu. Mkazo huu unatiliwa kwa sababu mtazamo wa kikuhani umeenea kwenye kitabu. Wafalme waliobaki wa Yuda wanajadiliwa, shinikizo likikazia jinsi maswala ya kidini yalikuwa yakienda. Hezekia anatajwa kwa njia ya kipekee kwa sababu wakati wa utawala wake uamsho wa muda mrefu ulifanyika. Kuharibiwa kwa Yerusalemu na uhamisho wa watu kwenda Babeli vinaelezewa. Kitabu kinamalizia kwa amri ya mfalme wa Uajemi ya kuachilia watu kurudi nyumbani.
Wazo Kuu
Historia ya Yuda inaelezewa kutokana na mtazamo wa kidini katika kitabu hiki.Wafalme waadilifu wanapongezwa, nao wafalme waovu wanatajwa ili wote wajue ni nani anahusika kuliinua au kuliangusha taifa. Viongozi wa kidini na kushindwa kwao kudumisha uaminifu kwa Mwenyezi Mungu kuliongeza kwa dhambi ya Yuda hadi Mungu akaruhusu watu wake waliochaguliwa kujiingiza katika maangamizi, wakiwa mfano wa wakati wote kwamba Mwenyezi Mungu hatastahimili dhambi.
Mwandishi
Hajulikani.
Tarehe
Karne ya 5 K.K.
Mgawanyo
• Utawala wa Sulemani (1:1–9:31)
• Kujengwa na kuwekwa wakfu kwa Hekalu (2:1–7:22)
• Utukufu wa utawala wa Sulemani (8:1–9:31)
• Wafalme wengine wa Yuda (10:1–36:23).