Utangulizi
Barua hii iliandikwa na Petro muda mchache tu kabla ya kifo chake na inashughulikia shida ambazo Petro aliona kwamba zitakuwepo hata baada ya kuondoka kwake. Anawatia moyo waumini kuendelea katika maisha yao ya kukua kiroho, huku wakitambua ukweli wa Injili ya Kikristo. Haihusishi hadithi bali ukweli. Anawaonya dhidi ya waalimu wa uongo ambao wataharibu ukweli kwa kuinua mawazo yao wenyewe juu ya mafundisho ya Kanisa. Mwishowe, anasema kwamba Al-Masihi atarudi siku moja kuharibu mfumo wa kale wa ulimwengu huu, na kwa ajili ya hilo, hatupaswi kushikamanishwa sana na ulimwengu.
Wazo Kuu
Kitabu cha 2 Petro ni mwito wa kusimama imara katikati ya misukumo kadhaa ya kupotosha ukweli. Ulimwengu unatafuta kudunisha kazi ya Mwenyezi Mungu, lakini lazima tupinge misukumo hii yote kwa kuishi maisha ya kiungu, kwa kuamini ukweli, kuvumilia mateso, kumtumainia Mwenyezi Mungu, na kutarajia kurudi kwa Al-Masihi.
Mwandishi
Mtume Petro.
Mahali
Hapajulikani, huenda ni Rumi.
Tarehe
Mwaka wa 66 B.K.
Mgawanyo
• Mbinu ya kukua kiroho (1:1-21)
• Maonyo dhidi ya waalimu wa uongo (2:1-22)
• Maneno ya kutia moyo, msingi wake ukiwa kurudi kwa Al-Masihi (3:1-18).