2 Wathesalonike Utangulizi
NMM

2 Wathesalonike Utangulizi

Utangulizi
Waraka wa kwanza wa Paulo ama barua gushi iliyosingiziwa kutoka kwake ilikuwa imewasumbua Wathesalonike kuhusu Al-Masihi kuja mara ya pili. Labda kilichochangia kuchanganyikiwa kwao ni mateso waliyokuwa wakipitia. Paulo anaandika ili kuwahakikishia waumini kwamba Al-Masihi kwa uhakika atarudi kuwafariji waumini na kuwaadhibu wanaowataabisha (1:7-8). Anawaambia pia siku kuu ya hukumu (siku ya Bwana) haitawapata kwa ghafula, bali itatanguliwa na msururu wa matukio (2:3). Katika ufahamu wa uhakika wa Al-Masihi kurudi, Wakristo wanatakiwa kuishi bila lawama.
Wazo Kuu
Katika waraka huu mfupi, ahadi ya Mwenyezi Mungu ya ushindi wake dhidi ya uovu imetiliwa mkazo.Waumini wanaweza kuteseka kwa sasa, lakini Mwenyezi Mungu amewapangia faraja na thawabu. Hata hivyo, kwa waliokataa kumtii Mwenyezi Mungu kutakuwa na huzuni na hukumu. Paulo anasisitiza umuhimu wa kuishi maisha ambayo yanamletea Mwenyezi Mungu heshima. Watu wengine kule Thesalonike walikuwa wameacha kufanya kazi kwa sababu waliamini kwamba Al-Masihi angerejea hivi karibuni. Hili jambo halileti heshima kwa Mwenyezi Mungu, na Paulo anasema hivi kulihusu, “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile” (3:10).
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Korintho.
Tarehe
51 B.K.
Mgawanyo
• Kuwafariji kupitia kurudi kwa Al-Masihi (1:1-12)
• Matukio kabla ya kuja kwa siku ya Bwana (2:1-12)
• Maagizo zaidi na maonyo (2:13–3:5)
• Tabia ya Kikristo, na salamu za mwisho (3:6-18).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu