Utangulizi
Amosi aliishi wakati mmoja na Hosea, Isaya, na Mika, na kama vile Hosea, ujumbe wake ulikuwa unalenga ufalme wa kaskazini wa Israeli, ingawa yeye mwenyewe alitoka ufalme wa kusini. Anaanza kwa kutangaza hukumu kwa mataifa yanayozunguka Israeli, na mwishowe kulenga Israeli yenyewe. Unafuata msururu wa shutuma kali dhidi ya dhambi za Israeli, haswa dhambi za kijamii za wakati ule, zikiwemo dhuluma, ufisadi katika viongozi, tamaa, na ibada isiyo ya kweli. Msururu wa maono unaendeleza ujumbe huu mkali, na kitabu kinamalizia kwa matumaini madogo mno kwamba Israeli itasikiliza.
Wazo Kuu
Msingi wa ujumbe wa Amosi ni mafundisho ya haki ya Mwenyezi Mungu ya milele. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, anadai haki kutoka kwa watu wake. Kama hawadhibitishi imani yao kwa maisha wanayoishi, hivyo basi watajibu kwa Mwenyezi Mungu. Msamaha unatolewa hata hivyo (5:6), na Israeli siku moja itarejeshwa kama ile ya zamani kwa uwezo na huruma za Mwenyezi Mungu.
Mwandishi
Amosi.
Tarehe
Karne ya 8 K.K.
Mgawanyo
• Utangulizi (1:1-2)
• Hukumu kwa mataifa na Israeli (1:3–2:16)
• Ujumbe wa nabii wa hukumu (3:1–6:14)
• Maono matano ya hukumu (7:1–9:10)
• Tumaini la wakati ujao (9:11-15).