Utangulizi
Paulo aliandika waraka huu akiwa mfungwa kule Rumi, ili kuwafariji na kuwatia moyo waumini wa Asia Ndogo. Anawapa maelezo ya jumla ya historia, akianzia mwanzo wa enzi Mwenyezi Mungu alipozindua mipango yake kwa ajili ya ulimwengu, hadi wakati wa sasa ambapo Mwenyezi Mungu anawaokoa wale waaminio Al-Masihi, na pia kwa siku zijazo wakati uovu wote utashindwa. Anaeleza ya kwamba kwa sasa kutakuwa na mvutano mkubwa kwa sababu tunapigana vita na nguvu za uovu au nguvu za giza (6:12). Lakini kwa sababu sisi ni viungo vya mwili wa Al-Masihi, tuna uwezo wa kustahimili. Kisha Paulo anashughulikia mambo halisi yanayohusiana na maisha ya Mkristo: ndoa, maadili na mienendo, wazazi na watoto, na pia watumishi.
Wazo Kuu
Wazo kuu katika Waefeso ni kwamba mpango wa Mwenyezi Mungu wa milele unafanyiwa kazi kupitia Al-Masihi na mwili wake, yaani kanisa. Mtu anapoamini, yeye yu ndani ya Al-Masihi na anapata wokovu na usalama. Mwenyezi Mungu alikuwa amepangia hili kutoka mwanzo, na amempa muumini kile chote anachohitaji kwa maisha yake ya Kikristo, lakini jukumu ni kwake kujipatia rasilimali anazohitaji kwa maisha. Paulo anamalizia barua kwa kuelezea vitu vya kujikimu ambavyo Mwenyezi Mungu ametoa kwa muumini ili aweze kustahimili mashambulizi makali ya Shetani, na vita vikiisha, awe mshindi.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Rumi.
Tarehe
Mwaka wa 60 au 61 B.K.
Mgawanyo
• Mpango wa Mungu, na wokovu wa muumini (1:1–2:22)
• Siri ya Injili (3:1-21)
• Maisha ya Mkristo duniani (4:1–5:21)
• Jinsi Wakristo wapaswavyo kuhusiana (5:22–6:9)
• Vita vya Mkristo dhidi ya uovu (6:10-24).