Utangulizi
Ezekieli alilelewa kama kuhani; alibebwa kwenda Babeli pamoja na Wayahudi waliotekwa mnamo 597 KK, na huko akawa nabii wa Mwenyezi Mungu. Ujumbe wake ulikuwa wa hukumu iliyokuwa inakuja kwa wale waliobaki Yerusalemu. Mahubiri yake hayakupokelewa vizuri na Wayahudi waliokuwa naye uhamishoni. Wakati utabiri wake wa kutisha ulipotimia mnamo 586 KK na kuharibiwa kwa Yerusalemu (ona 33:21), watu walimsikiliza kwanzia hapo kwa makini sana. Ujumbe wake ukabadilika pale kutoka kuwa wa hukumu isiopindwa, na kuwa ujumbe wa kufariji na kutia moyo kwa ajili ya siku za usoni. Mabaya zaidi yalikuwa yametukia; sasa ulikuwa wakati wa kufanya mpango kuanza tena. Ezekieli alijiona kama mchungaji na mlinzi kwa Israeli. Kama mchungaji alikuwa awalinde watu, lakini kama mlinzi alikuwa awaonye kwa hatari iliyokuwa mbele.
Wazo Kuu
Msingi wa ujumbe wa Ezekieli ni utakatifu wa Mwenyezi Mungu usiobadilika. Hii ni ahadi na onyo pia. Ni onyo kwa sababu Mwenyezi Mungu ameahidi kuhukumu dhambi, na hili halitabadilika. Ni ahadi kwa sababu Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa mwaminifu kwa watu wake, na hili halitabadilika. Kitabu cha Ezekieli kinaonyesha ahadi za Mwenyezi Mungu zisizovunjika zikitimizwa kwa hali zote mbili. Mji ulianguka kulingana na ahadi kwa sababu ya dhambi za Yuda; na mji utarejeshwa kulingana na ahadi kwa sababu ya uaminifu wa Mwenyezi Mungu. Maisha ya watu wa Mwenyezi Mungu yaliamua jinsi Mungu angewatendea.
Mwandishi
Ezekieli.
Tarehe
Karne ya 6 K.K.
Mgawanyo
• Mwito wa Ezekieli (1:1–3:27)
• Unabii dhidi ya Yuda na Yerusalemu (4:1–24:27)
• Unabii dhidi ya mataifa ya kigeni (25:1–32:32)
• Ahadi na matumaini ya kurejezwa (33:1–39:29)
• Hekalu lililofanywa upya katika Ufalme wa Mungu (40:1–48:35).