Wagalatia Utangulizi
NMM

Wagalatia Utangulizi

Utangulizi
Paulo aliwahubiria wenyeji wa Galatia katika safari yake ya kwanza ya kueneza Injili (Matendo 13:14–14:23). Muda mfupi baada ya kuondoka kwake, kikundi cha waumini wa Kiyahudi waliwasili huko na kusisitiza kwamba Wakristo wa Mataifa walipaswa kutii sheria za Musa ili wapate kuokolewa. Paulo anaandika ili kukabiliana na kosa hili kwa kuonyesha kwamba Ibrahimu, ambaye aliishi miaka 400 kabla ya Sheria kutolewa, aliokolewa kwa imani katika Injili. Kwa hivyo ilikuwaje kusema kwamba Sheria ingemwokoa mtu au kumfanya muumini katika Al-Masihi kuwa mtakatifu zaidi? Paulo anaunganisha hili na utetezi wa kina kuhusu mwito wake kama mtume na mjadla wa jinsi Mkristo anapaswa kuishi.
Wazo Kuu
Paulo anatetea ukweli wa Injili kwa moyo wote: ukweli huu ni kwamba mwanadamu huokolewa kwa neema ya Mwenyezi Mungu kupitia imani katika Al-Masihi, na hakuna zaidi. Mafunzo mengine yeyote yale ni ya kupotosha ukweli wa Mwenyezi Mungu (1:7). Tunafanyika haki mbele za Mwenyezi Mungu kwa imani (2:16), na kufanyika watu wa Mungu (yaani wana wa Ibrahimu) katika njia hiyo hiyo, kwa imani (3:7). Kwa kuwa tuko huru katika Al-Masihi, kamwe hatupaswi kumruhusu mtu yeyote kuturejesha nyuma katika dhana ya kuufanyia kazi wokovu wetu, lakini lazima tuishi kulingana na Injili. Hii inahusisha kutii Roho wa Mungu (5:16), na kuwapenda jirani zetu kama vile tunavyojipenda (5:14).
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Hapajulikani.
Tarehe
Kama 48 au 49 B.K.
Mgawanyo
• Paulo kujitetea, na pia kutetea Injili (1:1–2:21)
• Uhuru kutoka kwa laana ya Sheria (3:1-24)
• Ukuu wa Injili juu ya Sheria (3:25–4:31)
• Uhuru wa Mkristo (5:1-26)
• Himizo kuhusu maisha ya kawaida (6:1-18).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu