Utangulizi
Habakuki alihubiri wakati wa siku za mwisho za Yuda kabla ya kuanguka kwake mwaka wa 586 KK. Aliona maangamizi yaliyokuwa yanakaribia, na alitaabishwa na mambo mawili: Kwa nini Mwenyezi Mungu aliruhusu uovu kuwepo katika taifa la Yuda; na vile Mwenyezi Mungu angetumia taifa lenye dhambi kama Babeli kuadhibu Yuda kwa dhambi zake. Mwenyezi Mungu alijibu mkanganyo wa Habakuki kwa kumpa zaidi ya alichokiomba: alimpa maono ya Mwenyezi Mungu mwenyewe. Utambuzi huu mpya wa asili ya Mwenyezi Mungu na unyonge wake mwenyewe ulimpa Habakuki ujasiri wa kuishi katika siku hizo za giza kwa ushupavu na nguvu.
Wazo Kuu
Ukuu wa Mwenyezi Mungu na haja ya mwanadamu kumwamini ndio ujumbe mkuu katika kitabu hiki cha kusisimua. Mwenyezi Mungu ana madaraka juu ya mataifa yote, na atatenda lililo sahihi. Mwelekeo ufaao wa mwanadamu ni kumwamini, bali sio kuwa na shaka (2:4). Mwanadamu akifanya hivi, ataweza kuona zaidi ya ubaya wa mambo wa nje, na kuangalia maana ya ndani ya Mwenyezi Mungu, ili apate nguvu ya kuishi hata kutukie nini. Hatujui siku za usoni, lakini Mwenyezi Mungu anajua na anaweza kuaminika kabisa.
Mwandishi
Habakuki.
Tarehe
Karne ya 7 K.K.
Mgawanyo
• Dhambi na adhabu (1:1-11)
• Babeli na Mwenyezi Mungu (1:12–2:20)
• Imani ya ushindi ya Habakuki (3:1-19).