Utangulizi
Hagai alihudumu wakati mmoja na Zekaria, na alitumwa na Mwenyezi Mungu kuhubiria jumuiya iliyorejeshwa na kuwatia moyo kumaliza kazi ya kujenga Hekalu tena. Jumbe zake zilielekezwa kwa viongozi wawili wa watu, yaani Zerubabeli aliyekuwa mtawala, na Yoshua aliyekuwa kuhani. Kitabu kinahusisha jumbe tano za kinabii ambazo zilikusudiwa kuharakisha kazi. Jumbe hizi zilitenda kama zilivyotakiwa, na Hekalu liliwekwa wakfu mnamo 516 K.K.
Wazo Kuu
Wazo kuu la kitabu hiki ni kuhusika kwa Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu wake, na pia kuonyesha kwamba mambo ya kiroho ni ya maana. Watu walikuwa wameacha kazi ya kujenga Hekalu, wakashughulikia mambo yao binafsi, lakini Mwenyezi Mungu alitaka waone kwamba mahala pa kuabudu sharti patengenezwe kwa wema wa taifa lao. Malalamiko kwamba Hekalu jipya halingekuwa na utukufu kama la kwanza yalikomeshwa na ahadi ya Mwenyezi Mungu kwamba yeye angelijaza na utukufu wake (2:7).
Mwandishi
Hagai.
Tarehe
Mwaka wa 520 K.K.
Mgawanyo
• Nabii kuwakemea watu kwa kuachilia Hekalu (1:1-11)
• Kibali cha Mwenyezi Mungu (1:12-15)
• Wajenzi kutiwa moyo (2:1-9)
• Baraka zitakazofuata kazi (2:10-19)
• Ushindi wa Mungu dhidi ya mataifa (2:20-23).