Utangulizi
Kitabu cha Hosea kinahusisha sehemu mbili zisizotoshana: ya kwanza ni maisha ya Hosea (1–3), nayo ya pili ni jumbe za Hosea (4–14). Hosea alikuwa nabii katika ufalme wa kaskazini wa Israeli kabla haujaangamizwa mnamo 722 K.K., na huduma yake ilichukua muda wa miaka 40. Alihubiri wakati mmoja na Amosi, Isaya, na Mika. Maisha ya kuhuzunisha ya nyumbani mwa Hosea yalikuwa mfano wa hali ya nchi yake. Kama vile mkewe aliondoka nyumbani na kuishi maisha ya ukahaba, ndivyo Israeli walikuwa wamemwacha Mwenyezi Mungu ili kutafuta miungu ya uongo. Lakini kama vile Hosea aliendelea kumpenda mkewe na mwishowe akamrudisha nyumbani, ndivyo Mwenyezi Mungu aliendelea kupenda Israeli na akaahidi kuwarejesha siku moja katika hali ya kukubalika tena.
Wazo Kuu
Mambo mawili yanaonekana yakiwa kinyume moja kwa kingine. Haya ni upendo wa Mwenyezi Mungu, na uasi wa Israeli. Mwenyezi Mungu anaonyeshwa akiwa mwaminifu, anayejali, anayesamehe, mkarimu na mwenye upendo. Upendo wa Mwenyezi Mungu usiokoma ndilo wazo kuu la kitabu hiki. Israeli wanaonekana hawana uaminifu, wanapotoka, wenye dhambi, waasi, na wazinzi. Israeli hawafahamu ushindi unatokea wapi mwishowe, lakini upendo wa Mwenyezi Mungu utatenda muujiza wa kurejeza Israeli.
Mwandishi
Hosea.
Tarehe
Karne ya 8 K.K.
Mgawanyo
Maisha ya kuhuzunisha ya nyumbani kwa Hosea (1:1–3:5)
Uasi wa Israeli dhidi ya Mwenyezi Mungu (4:1–8:14)
Hukumu inayokuja (9:1–13:16)
Kurejezwa kunaahidiwa (14:1-9).