Isaya Utangulizi
NMM

Isaya Utangulizi

Utangulizi
Huduma ndefu ya Isaya ilichukua karibu miaka sitini wakati wa utawala wa wafalme wanne, wa mwisho akiwa Hezekia, aliyeleta mabadiliko makuu. Isaya alitumwa hasa katika Yuda, ijapokuwa ujumbe wake ulikuwa kwa Ufalme wa Kaskazini mwa Israeli pia. Aliishi siku mbaya za vita vya ndani kati ya Israeli na Yuda mnamo 734-732 KK. Somo kuu kutokana na kuanguka kwa Israeli lilikuwa ni mafundisho kwake Isaya, na alitumia somo hilo kumtia moyo Hezekia kuweka tumaini lake ndani ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu alikomboa Yuda kutokana na jeshi kubwa la Ashuru kwa kutuma pigo kuwaua katika kambi. Isaya pia aliona baada ya siku zake hadi wakati utakaokuja wa uhamisho wa Yuda na wokovu ambao Mwenyezi Mungu angepeana.
Wazo Kuu
Kitabu cha Isaya kilikuwa mojawapo wa vitabu alivyopenda Yesu na alikinukuu mara nyingi, kwa sababu maudhui kuu ni wokovu. Mwenyezi Mungu anaonekana kama Mwokozi wa watu wake, aliyewakomboa kutoka Misri, atakayewaokoa kutoka kwenye kutekwa kunaokuja, na atamtuma Mtumishi wake mpendwa kubeba dhambi zetu sote (53:6). Mwenyezi Mungu anatoa msamaha bure kwa wote ambao wanakuja kwake kwa toba na imani. Ufalme ujao wa Mwenyezi Mungu duniani pia unaelezewa kwa kina kama wakati ambao wanadamu wataweka silaha chini, na wataimba kwa amani nyimbo za kusifu Mwenyezi Mungu, mfalme wao.
Mwandishi
Isaya.
Tarehe
Karne ya 8 K.K.
Mgawanyo
• Unabii kuhusu Yuda na mataifa (1:1–23:18)
• Hukumu ya Mungu juu ya dhambi za dunia (24:1–27:13)
• Unabii kuhusu Yuda na Israeli (28:1–35:10)
• Maisha ya Isaya wakati wa utawala wa Hezekia (36:1–39:8)
• Kufarijiwa kwa siku zijazo kwa Yuda, na wokovu wa Mungu (40:1–66:24).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu