Yohana 4
NMM

Yohana 4

4
Isa Azungumza Na Mwanamke Msamaria
1 # Yn 3:22-26 Mafarisayo wakasikia kwamba Isa alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yahya, 2#1Kor 1:17ingawa kwa kweli si Isa mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. 3#Yn 3:22Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya.
4 # Lk 9:52 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. 5#Mwa 48:22; Yos 24:32Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. 6Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7 # Mwa 24:17; 1Fal 17:10 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.” 8#Yn 4:5, 30(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9 # Mt 10:5; Lk 9:52-53 Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.
10 # Isa 55:1; Ufu 21:6 Isa akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”
11Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12#Yn 4:6; 8:53Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”
13 # Yn 6:58 Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki, ataona kiu tena. 14#Yn 6:35; Isa 12:3; Yn 7:38; Mt 25:46Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.”
15 # Yn 6:34 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”
16Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”
17Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”
Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. 18Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”
19 # Mt 21:11 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. 20#Kum 11:29; Yos 8:33; Lk 9:53; 4:21; 4:20; Yn 5:28; 16:2; 1Tim 2:8Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”
21 # Yn 5:28; 16:2; Mal 1:11; 1Tim 2:8 Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22#2Fal 17:28-41; Isa 2:3; Rum 9:4-5Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23#Yn 5:25; 16:32; Flp 3:3Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24#Flp 3:3Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
25 # Mt 1:16; Yn 1:41 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Al-Masihi) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”
26 # Yn 8:24; 9:35-37 Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”
27 # Yn 4:8 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?”
28Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu, 29#Mt 12:23; Yn 7:26, 31“Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Al-Masihi?”#4:29 Al-Masihi maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. 30Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Isa.
31 # Mt 23:7 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.”
32 # Ay 23:12; Mt 4:4 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”
33Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” 34#Mt 26:39; Yn 17:4; 19:30Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. 35#Mt 9:37; Lk 10:2Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36#Rum 1:13; Mt 25:46Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37#Ay 31:8; Mik 6:15Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
Wasamaria Wengi Waamini
39 # Yn 4:29 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” 40Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. 41Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
42 # Lk 2:11; 1Yn 4:14 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.”
Isa Amponya Mwana Wa Afisa
43Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. 44#Mt 13:57; Lk 4:24(Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) 45#Yn 2:23Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
46 # Yn 21:1-11 Hivyo Isa akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47#Yn 4:3, 54; Lk 7:2Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
48 # Dan 4:2-3; Ebr 2:4 Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
49Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
50Isa akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.”
Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaondoka akaenda zake. 51Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”
53 # Mdo 11:14 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye, pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.
54 # Yn 4:8; 2:11 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu