Ayubu 30
NMM

Ayubu 30

30
1 # Ay 12:4; Za 119:21 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki,
watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau
kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
2Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,
kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3 # Isa 8:21; Ay 24:5; Yer 17:6 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,
walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
4 # Ay 39:6; 1Fal 19:4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi,
nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
5Walifukuzwa mbali na watu wao,
wakipigiwa kelele kama wevi.
6 # Isa 2:19; Hos 10:8 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,
kwenye majabali na mahandaki.
7 # Ay 6:5; 39:5-6 Kwenye vichaka walilia kama punda,
na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
8 # Amu 9:4; Ay 18:18 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,
waliofukuzwa watoke katika nchi.
9 # Ay 16:10; 12:4; Za 69:11; Mao 3:14; Ay 16:10; Za 69:11; Ay 12:4; Mao 3:14, 63; Ay 17:6 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo;
nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10 # Hes 12:14; Mt 26:67 Wananichukia sana na kujitenga nami,
wala hawasiti kunitemea mate usoni.
11 # Mwa 12:17; Rut 1:21; Ay 41:13; Za 32:9 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa,
wamekuwa huru kunitendea waonavyo.
12 # Za 109:6; Zek 3:1; Za 140:4-5; Ay 16:10 Kuume kwangu kundi linashambulia;
wao huitegea miguu yangu tanzi,
na kunizingira.
13 # Isa 3:12; Za 69:26 Huizuia njia yangu,
nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,
nami sina yeyote wa kunisaidia.
14Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana;
katikati ya magofu huja na kunishambulia.
15 # Kut 3:6; Za 55:4-5; Hos 13:3; Ay 3:25 Vitisho vimenifunika;
heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,
salama yangu imetoweka kama wingu.
16 # Za 22:14; Isa 53:12 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho;
siku za mateso zimenikamata.
17Usiku mifupa yangu inachoma;
maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
18Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;
hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
19 # Za 40:2; Yer 38:6, 22 Yeye amenitupa kwenye matope,
nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
20 # Ay 19:7; Mao 3:8; Mt 15:23 “Ee Bwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu;
ninasimama, nawe unanitazama tu.
21 # Ay 19:6; Yer 6:23; Isa 9:12; Eze 6:14; Ay 10:3 Wewe unanigeukia bila huruma;
unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
22 # Ay 27:21; 9:17; Yud 1:12 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo;
umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.
23 # 2Sam 14:14; Ay 3:19; 10:8 Ninajua utanileta mpaka kifoni,
mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.
24“Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji,
anapoomba msaada katika shida yake.
25 # Za 35:13-14; Rum 12:15; Yn 11:35 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?
Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
26 # Za 82:5; Yer 8:15 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;
nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
27 # Za 38:8; Mao 2:11 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii;
siku za mateso zinanikabili.
28 # Mao 4:8; Za 38:6; Ay 19:7; 24:12 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua;
ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
29 # Isa 34:13; Yer 9:11; Za 102:6; Mik 1:8 Nimekuwa ndugu wa mbweha,
rafiki wa mabundi.
30 # Mao 3:4; 4:8; 5:10; Kum 28:35 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika;
mifupa yangu inaungua kwa homa.
31 # Mwa 8:8; Za 137:2 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,
nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu