Maombolezo Utangulizi
NMM

Maombolezo Utangulizi

Utangulizi
Kitabu cha Maombolezo ni wimbo wa kuomboleza, ulioandikiwa mji ulioanguka wa Yerusalemu. Wimbo huu ulitungwa na Yeremia, ambaye alikuwa shahidi wa mambo ambayo anayaelezea kwa kina kikubwa. Anaonyesha uharibifu uliotokea kwa hali ya kutisha ili kamwe kusiwahi kuulizwa tena: “Kwa nini hakuna yeyote aliyethubutu kututahadharisha kuhusu gharama kubwa ambayo tungelipa kwa kutomtii Mwenyezi Mungu?”
Kuna kiasi kidogo cha faraja, lakini maombi ya Yeremia katika sura ya tano yanaangazia zaidi ya uharibifu ya mji wa Yerusalemu, ambao hapo awali ulikuwa mji wa fahari wa Mwenyezi Mungu ambaye enzi yake inadumu milele. Ni hapo tu ndipo Yeremia anaweza kupata faraja yoyote.
Wazo Kuu
Kitabu cha Maombolezo ni tangazo la gadhabu ya Mwenyezi Mungu. Kinaonyesha ukweli mchungu kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa ameahidi hukumu dhidi ya dhambi, nao watu wa Yuda walikuwa wapumbavu kiasi cha kumjaribu Mwenyezi Mungu. Licha ya kuwa jambo mbaya kadri lilivyoonekana, la kusikitisha kabisa lilikuwa kwamba halikupaswa kutokea. Uaminifu wa Mwenyezi Mungu ni mkuu, ukifanywa upya kila asubuhi, na rehema zake hazina kikomo (3:22-23).
Mwandishi
Yeremia.
Tarehe
Karne ya 6 K.K.
Mgawanyo
• Huzuni ya Yerusalemu na uharibifu (1:1-22)
• Hasira ya Mungu kwa ajili ya dhambi ya Yerusalemu (2:1-22)
• Tumaini pekee la Yerusalemu ni rehema za Mungu (3:1-66)
• Utukufu wa Yerusalemu wa hapo mwanzo, na aibu yake ya wakati huu (4:1-22)
• Maombi ya ukombozi wa Yerusalemu (5:1-22).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu