Luka 5
NMM

Luka 5

5
Kuitwa Kwa Wanafunzi Wa Kwanza
(Mathayo 4:18-22; Marko 1:16-20)
1 # Mk 4:14; Ebr 4:12 Siku moja Isa alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti,#5:1 Yaani Bahari ya Galilaya. watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu, 2akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. 3#Mt 13:2Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.
4 # Yn 21:6 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”
5 # Lk 9:33, 49; Lk 17:13; Yn 21:3 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”
6 # Yn 21:11 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. 7Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.
8 # Mwa 18:27; Ay 42:6 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Isa na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” 9Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10#Mt 14:27Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.
Ndipo Isa akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” 11#Mt 4:11Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.
Isa Amtakasa Mtu Mwenye Ukoma
(Mathayo 8:1-4; Marko 1:40-45)
12 # Mt 8:12 Ikawa siku moja Isa alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Isa, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”
13Isa akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika.
14 # Mt 8:4 Isa akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
15 # Mt 9:26 Lakini habari zake Isa zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16#Mt 14:23Lakini mara kwa mara Isa alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.
Isa Amponya Mtu Mwenye Kupooza
(Mathayo 9:1-8; Marko 2:1-12)
17 # Mt 15:1; Lk 2:46; Mk 5:30; Lk 6:19 Siku moja Isa alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. 18#Mt 9:2; Mk 2:8Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Isa. 19Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya ule umati pale mbele ya Isa.
20 # Lk 7:48-49 Isa alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”
21 # Isa 43:25; Lk 7:49; Yn 5:12 Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
22Isa akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 23Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 24#Mt 8:20Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 25Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. 26#Mt 9:8Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”
Isa Amwita Lawi
(Mathayo 9:9-13; Marko 2:13-17)
27 # Mt 4:19 Baada ya haya, Isa alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” 28#Lk 5:11; Mt 4:19Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
29 # Lk 15:1 Kisha Lawi akamfanyia Isa karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao. 30#Mdo 23:9; Mt 9:11Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Isa, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
31Isa akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32#Yn 3:17Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”
Isa Aulizwa Kuhusu Kufunga
(Mathayo 9:14-17; Marko 2:18-22)
33 # Lk 7:18; Yn 1:35; 3:25-26; Mt 14:17; Mk 2:18-22 Wakamwambia Isa, “Wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”
34 # Yn 3:29; Mt 14:17; Mk 2:18-22 Isa akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao? 35#Lk 9:22; 7:22; Mt 14:17; Mk 2:18-22Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”
36 # Mt 14:17; Mk 2:18-22; Mt 9:16, 17; Mk 2:21, 22 Isa akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa. 37#Mt 14:17; Mk 2:18-22Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika. 38#Mt 14:17; Mk 2:18-22Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya. 39#Mt 14:17; Mk 2:18-22Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, bali husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu