Utangulizi
Luka alikuwa tabibu ambaye alisafiri na Mtume Paulo katika safari zake. Aliandika Injili hii kwa Myunani aliyeitwa Theofilo (1:3) ili kuonyesha ubinadamu halisi wa Isa na mahali pake katika historia. Kwa ajili ya hili, Luka alikuwa mwangalifu katika kutafiti ushahidi wote kwa makini, na kutoa tarehe kamili za matukio yaliyotokea. Anaanza kwa kuelezea kuzaliwa kwa Isa na bikira, akitoa habari kwa mapana ambazo hazipatikani kwingine. Huduma ya Isa huko Galilaya inaelezewa, ikifuatwa na maelezo marefu ya safari ya Isa kuelekea Yerusalemu. Baada ya kufa na kufufuka kwa Isa, wanafunzi wanaachwa wakifurahia, wakisubiri ahadi ya nguvu za Mwenyezi Mungu itakayowajilia kuwajaza kutoka mbinguni.
Wazo Kuu
Ilhali Mathayo anamwonyesha Isa kuwa Masiya wa Wayahudi na Marko anamwonyesha kama mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Luka anamwelezea Isa kama Mungu na pia Mwanadamu ambaye uzao wake unatoka kwa Ibrahimu (3:23-28). Isa ndiye mwanadamu mkuu zaidi katika historia, na Luka anamweka katikati ya mfululizo wa matukio ya dunia. Yeye ndiye mwanadamu mkuu zaidi kutokana na yale aliyafunza, yale alitenda, sababu yake kufa, na zaidi ya yote kwa sababu alifufuka kutoka kwa wafu. Kwa hivyo, tunapaswa kumkubali kuwa Bwana wetu.
Mwandishi
Luka.
Mahali
Huenda ni Kaisaria.
Tarehe
Kama mwaka wa 60-65 B.K.
Mgawanyo
• Kuzaliwa kwa Isa na ujana wake (1:1–2:52)
• Kubatizwa na kujaribiwa kwa Isa (3:14–4:13)
• Huduma ya Isa huko Galilaya (4:14–9:50)
• Safari ya Isa kwenda Yerusalemu (9:51–19:27)
• Huduma ya Isa huko Yerusalemu (19:28–20:47)
• Unabii kuhusu mambo yajayo (21:1-38)
• Kufa na kufufuka kwa Isa (22:1–24:53).