Utangulizi
Malaki alitumwa kama nabii kwa jamii iliyorejeshwa wakati ambao moto wao wa kiroho ulikuwa chini kabisa. Nehemia na Ezra walikuwa wameanzisha ibada muhimu na mabadiliko ya kisiasa, na Malaki alikuwa akiwaongoza watu kushughulikia matatizo yao ya kiroho. Matatizo makuu ambayo Malaki anagusia ni ufisadi wa makuhani, kuachiliwa kwa Hekalu la Mungu, na dhambi binafsi nyumbani. Anamalizia kitabu hiki kwa unabii kuhusu kuja kwa Masiya, na mtangulizi wake Yahya Mbatizaji (anayeitwa Ilya hapa). Hivyo basi kitabu hiki cha mwisho kati ya Manabii kinaishia kikitazamia yale Mwenyezi Mungu atatenda katika Injili.
Wazo Kuu
Watu hawajajifunza somo la uhamishoni. Walikuwa wametumwa uhamisho kwa sababu ya dhambi zao, na sasa walikuwa wakiyarudia mambo yale yale. Talaka ilikuwa kawaida, watu walikuwa wabinafsi na waongo, Hekalu lilikuwa limetelekezwa, na kulikuwa na hali ya kushuka kiroho kila mahali. Malaki anawalaumu viongozi wa kidini kwa sababu kati ya watu wote wao walitakiwa kujua kile ambacho Mwenyezi Mungu anahitaji kwao. Malaki anapata tumaini katika kuja kwa Masiya ambaye atarekebisha mambo yote kwa sababu anakuja na uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Mwandishi
Malaki.
Tarehe
Kama 450-425 K.K.
Mgawanyo
• Upendo wa Mwenyezi Mungu na aibu ya Israeli (1:1–2:9)
• Dhambi ya Israeli yakemewa (2:10–2:17)
• Hukumu ya baadaye yatabiriwa (3:1-6)
• Zaka iliyopuuzwa (3:7-18)
• Kuja kwa Isa kwatabiriwa (4:1-6).