Mathayo Utangulizi
NMM

Mathayo Utangulizi

Utangulizi
Mathayo alikuwa mtoza ushuru ambaye Bwana Isa alimwita awe mwanafunzi wake hapo mwanzoni mwa huduma yake ya hadharani. Kwa hivyo alikuwa shahidi wa macho wa matukio mengi anayoelezea. Anaanza kwa maelezo ya kina ya Isa alivyozaliwa na Bikira Mariamu, alivyobatizwa, na kujaribiwa nyikani. Isa alikuja akihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu, ambao ni wa kila mtu anayetaka kupata uzima wa milele. Mtu anaingia katika Ufalme huu kwa kutubu dhambi na kumwamini Isa. Mathayo aliyagawa mafundisho ya Isa katika sehemu kuu tano ambazo zinaonyesha maadili ya Ufalme wa Mungu, kutangaza Injili, mifano, ushirika, na kuja kwa Ufalme wa Mungu. Sehemu ya mwisho ya Injili ya Mathayo inaeleza juu ya kufa na kufufuka kwa Isa, na agizo alilolitoa kwa wote wanaomwamini kueneza Habari Njema ya Isa Al-Masihi ulimwenguni kote.
Wazo Kuu
Lengo kuu la Mathayo kuandika Injili hii ni kuonyesha kwamba Isa anatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu katika Torati ya Musa, Manabii, na Zaburi. Kwa sababu hii, Isa anatambulishwa kama “mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu” (1:1). Mathayo anatumia utabiri mwingi na nukuu kutoka Torati, Manabii na Zaburi kuelezea maisha ya Isa. Isa alikuja kuwa Mwokozi wa Wayahudi (1:21), watu wa Mataifa (4:13-16), na hatimaye wa dunia (28:19). Maadili yanayotakiwa kwa wafuasi wa Ufalme wa Mungu yanapatikana katika Mahubiri ya Isa kwenye Mlima (5–7), ambapo maadili ya dunia yanakataliwa, nao Ufalme wa Mungu na haki yake zinainuliwa juu ya vyote (6:33).
Mwandishi
Mathayo.
Mahali
Pengine Antiokia.
Tarehe
Kati ya 60-70 B.K.
Mgawanyo
• Maisha na huduma ya awali ya Isa (1:1–4:25)
• Mahubiri ya Mlimani (5:1–7:29)
• Mafundisho, mafumbo na hotuba (8:1–18:35)
• Safari ya kwenda Yerusalemu, na maonyo ya mwisho (19:1–23:39)
• Unabii kuhusu mambo yajayo (24:1–25:46)
• Kufa na kufufuka kwa Isa (26:1–28:20).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu