Utangulizi
Mika aliishi wakati mmoja na Isaya, na alihubiri kwa falme zote mbili za Israeli na Yuda katika karne ya 8 KK. Aliishi katika mji mdogo wa Moreshethi uliokuwa kusini mwa Yerusalemu, ila alielekeza ujumbe wake kwa miji mikuu ya Yerusalemu na Samaria. Anakemea uonevu wao, majivuno, uchoyo, ufisadi, kujifanya watakatifu kwao, na ufidhuli. Kama viongozi wa taifa, miji hiyo mikuu inatakiwa kuongoza katika uadilifu, bali sio katika dhambi, na Mwenyezi Mungu mwenye haki atahitaji wawajibike kwa matendo yao.
Wazo Kuu
Uadilifu wa Mwenyezi Mungu na wanadamu kuhitajika na Mwenyezi Mungu kuwa waadilifu ndio ujumbe mkuu katika kitabu hiki. Mwenyezi Mungu anadai haki, unyenyekevu na upendo kutoka kwa watu wake, sio kujionyesha kwa nje tu (6:8). Wale ambao wanaendelea katika uasi, uonevu na majivuno watahukumiwa na Mwenyezi Mungu. Mika pia anatabiri kuja kwa Al-Masihi na pia mahali pa kuzaliwa kwake (5:2). Unabii huu ulikumbukwa na washauri wa Herode wakati wataalamu wa nyota walikuwa wanamtafuta mtoto Isa (Mathayo 2:4-6).
Mwandishi
Mika.
Tarehe
Karne ya 8 K.K.
Mgawanyo
• Hukumu ya Mwenyezi Mungu (1:1-16)
• Mwenyezi Mungu kuchukia dhambi (2:1–3:12)
• Baraka za siku zijazo (4:1–5:1)
• Kuja kwa Masiya (5:2-15)
• Hukumu ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Israeli (6:1–7:20).