Marko 12
NMM

Marko 12

12
Mfano Wa Wapangaji Waovu
(Mathayo 21:33-46; Luka 20:9-19)
1 # Isa 5:17 Isa akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akachimba shimo ndani yake kwa ajili ya shinikizo la kusindika divai, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwenda nchi nyingine. 2Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji. 3Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. 4Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu. 5Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.
6 # Ebr 1:1-3 “Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
7“Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’ 8#Ebr 13:12Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
9“Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu. 10#Mdo 4:11Je, hamjasoma Andiko hili:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
11 # Za 119:22-23 Bwana ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni ajabu machoni petu’?”
12 # Mk 11:18; Mt 22:22 Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa ule umati wa watu. Wakamwacha, wakaondoka, wakaenda zao.
Swali Kuhusu Kulipa Kodi
(Mathayo 22:15-22; Luka 20:20-26)
13 # Mt 22:16; Mk 3:6; Mt 12:10 Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kwenda kumtega Isa katika yale anayosema. 14Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? 15Je, tulipe kodi au tusilipe?”
Lakini Isa alijua unafiki wao. Akawauliza “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari#12:15 Dinari moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. niione.” 16Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
17 # Rum 13:7 Ndipo Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
Nao wakamstaajabia sana.
Ndoa Wakati Wa Ufufuo
(Mathayo 22:23-33; Luka 20:27-40)
18 # Mdo 4:1; Mdo 23:8; 1Kor 15:12 Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa, 19#Kum 25:5wakasema, “Mwalimu, Musa alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 20Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa pasipo kuwa na mtoto yeyote. 21Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. 22Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa. 23Kwa hiyo wakati wa ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
24 # 2Tim 3:15-17 Isa akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu? 25#1Kor 15:42, 49, 52Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26#Kut 3:6Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Musa jinsi Mungu alivyosema na Musa kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?’ 27Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
Amri Iliyo Kuu
(Mathayo 22:34-40; Luka 10:25-28)
28 # Lk 10:25-28; Lk 20:39 Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Isa amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29 # Kum 6:4; Lk 10:27 Isa akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mwenyezi Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 30#Kum 6:4-5Mpende Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ 31#Law 19:18; Mt 5:43Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32 # Kum 4:35-39; Isa 46:9 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Isa, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33#Hes 6:6; Ebr 10:8Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34 # Mt 3:2; Mt 22:46; Lk 20:40 Isa alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
Al-Masihi Ni Mwana Wa Nani?
(Mathayo 22:41-46; Luka 20:41-44)
35 # Mt 26:55; Mt 9:27 Isa alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa sheria wanasema kwamba Al-Masihi#12:35 Al-Masihi maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. ni Mwana wa Daudi? 36#2Sam 23:2; Za 110:1; Mt 22:24Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, alisema:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
37 # Yn 12:9 Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”
Ule umati wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
Isa Awatahadharisha Watu Kuhusu Walimu Wa Sheria
(Mathayo 23:1-36; Luka 20:45-47)
38 # Mk 4:2; Mt 23:1; Lk 20:46; Lk 11:43 Alipokuwa akifundisha, Isa alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39#Lk 11:43Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40#Mt 23:14Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
Sadaka Ya Mjane
(Luka 21:1-4)
41 # 2Fal 12:9; Yn 8:20 Kisha Isa akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 # 2Kor 8:12 Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44#2Kor 8:12Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu