Utangulizi
Yohana Marko alikuwa mshirika wa Mtume Paulo. Mwishowe alihamia Rumi ambapo aliandika ukumbusho wa habari za Mtume Petro. Kwa hivyo Injili ya Marko inatoa habari za mtu anayeelezea mambo ambayo aliyashuhudia kwa macho. Kusudi la Marko lilikuwa kuweka pamoja ujumbe wa kina wa Injili. Anakazia matendo ya Al-Masihi zaidi ya maneno yake, na anatenga nafasi kubwa sana kuelezea matukio ya juma la mwisho la Isa. Injili ya Marko inaanza na huduma ya Isa hadharani, na kuhubiri kwake kwa Injili ya Ufalme wa Mungu. Kifo chake kinatabiriwa kwa wazi mara kadhaa (8:31; 9:31; 10:33-34, 45), na kisha Isa anaelekea msalabani kufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.
Wazo Kuu
Marko anamwelezea Isa kama Mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyekuja kufanya mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Miujiza, uponyaji, ushindi juu ya mapepo, na nguvu zake binafsi zote zinaonyesha ulimwengu kwamba hakuwa mtumishi wa kawaida tu, lakini pia alikuwa kweli Mwana wa Mwenyezi Mungu (15:39). Kufufuka kwa Isa kulithibisha yote aliyokuwa akifanya, na sasa tunangoja kurudi kwake kwa utukufu kutoka mbinguni. Marko pia aliandika ili kuwatia moyo Wakristo wa Rumi katika kipindi cha mateso.
Mwandishi
Marko.
Mahali
Rumi.
Tarehe
Kati ya 55-65 B.K.
Mgawanyo
• Yahya Mbatizaji, na ubatizo wa Bwana Isa (1:1-13)
• Huduma ya Isa huko Galilaya (1:14–9:50)
• Safari ya kwenda Yerusalemu na kuingia mjini (10:1–11:25 [26])
• Vurugu katika mji (11:27–12:44)
• Unabii kuhusu mambo yajayo (13:1-37)
• Kifo cha Isa, na kufufuka kwake (14:1–16:8 [20]).