Utangulizi
Kitabu hiki kinazungumzia kuhusu safari ya Israeli kutoka Mlima Sinai hadi katika mpaka wa Kanaani, na kujiandaa kwa Waisraeli kuingia katika nchi. Hata hivyo, kwa sababu ya dhambi na kutoamini, hawakuruhusiwa na Mwenyezi Mungu kudai urithi wao, lakini walihukumiwa kuhangaika jangwani kwa miaka arobaini. Baada ya miaka arobaini, walienda taratibu katika safari ya kuingia Kanaani; wakati huu walikuwa tayari kutii amri za Mwenyezi Mungu. Baada ya kushinda baadhi ya vita muhimu mashariki mwa Mto Yordani, Waisraeli walijiandaa ili kuingia katika nchi yenyewe.
Wazo Kuu
Kitabu hiki kinaonyesha uaminifu wa Mwenyezi Mungu usio na kikomo, na dhambi zilizokithiri za mwanadamu. Israeli walimkataa Mwenyezi Mungu, lakini Mungu alizidi kuwa mwaminifu kwa ahadi yake, kwa kuwaongoza jangwani na kutimiza mahitaji yao. Katika Injili, maisha ya Ukristo yanafananishwa na kuhangaika jangwani, kukifuatwa na ahadi ya mbingu ya Kanaani iliyo mbele yetu (Waebrania 3:7-9; 4:8-11).
Mwandishi
Musa.
Tarehe
Mwaka wa 1420 au 1220 K.K.
Mgawanyo
• Kuhesabiwa kwa wanaume kwa ajili ya vita (1:1–2:34)
• Kanuni maalum za maisha ya Israeli (3:1–10:10)
• Safari ya kwenda Kanaani, na uasi mkuu uliotokea (10:11–14:45)
• Kuhangaika jangwani (15:1–19:22)
• Safari ya kuelekea Moabu, na kisa cha Balaamu (20:1–25:18)
• Maandalio ya kuingia Kanaani yaliyofanywa Moabu (26:1–36:13).