Wafilipi Utangulizi
NMM

Wafilipi Utangulizi

Utangulizi
Paulo aliandika barua hii akiwa gerezani huko Rumi, kwa marafiki zake wa karibu mno huko Filipi. Alikuwa akiwapongeza kwa kumtumia pesa za kumsaidia kwa mahitaji yake. Anaanza kwa kuelezea imani yake kwao, kisha anashiriki baadhi ya shida anazokumbana nazo huko Rumi. Kama atakufa au la hajui, lakini ikiwa kifo kitamjia, atafurahia katika uwepo wa Al-Masihi. Ikiwa atakuwa hai, ataendelea kumtumikia Mwenyezi Mungu kadri anavyoweza.
Mfano wa unyenyekevu wa Al-Masihi unatolewa kwa Wafilipi kama mfano wa kufuatwa. Waalimu wa uongo wapaswa kukataliwa kabisa. Kina dada wawili wanaogombana wanashauriwa kupatana. Mwishowe waumini wanahimizwa kuweka viwango vya juu vya maadili maishani mwao kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakutana na mahitaji yote ambayo mtu anayo maishani.
Wazo Kuu
Katika barua hii ya kibinafsi ya Paulo, somo kuu la kufurahia linajitokeza kila mahali. Ikiwa mtu ataishi, anaweza kufurahia kwa kuwa Mwenyezi Mungu anampenda, naye Al-Masihi alimfia, na mambo yote yanatolewa kwake na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maisha yake. Ikiwa mtu atakufa, basi anaweza kufurahia kwa kuwa katika uwepo wa Al-Masihi milele. Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba Wakristo hawatakuwa na shida. Kama vile ilivyombidi Al-Masihi kuvumilia msalaba, pia sisi lazima tuwe tayari kufuata mfano huo wa kunyenyekea mbele za Mwenyezi Mungu, ikiwa ni lazima iwe hivyo. Lakini sisi ni raiya wa mbinguni (3:20) na twapaswa kuishi na wazo hilo kila mara mioyoni mwetu.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Rumi.
Tarehe
Kama mwaka wa 61 B.K.
Mgawanyo
• Paulo na shida zilizokuwa Rumi (1:1-30)
• Mfano wa unyenyekevu wa Al-Masihi (2:1-30)
• Maonyo na himizo za maisha yafaayo ya Ukristo (3:1-21)
• Amani ya Mungu, na upaji wa Mungu kwa muumini (4:1-23).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu