Mithali 18
NMM

Mithali 18

18
1Mtu ajitengaye na wengine
hufuata matakwa yake mwenyewe;
hupiga vita kila shauri jema.
2 # Mit 12:23 Mpumbavu hafurahii ufahamu,
bali hufurahia kutangaza
maoni yake mwenyewe.
3Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia,
pamoja na aibu huja lawama.
4 # Za 18:16 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji,
bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.
5 # Law 19:15; Mit 28:21; Za 82:2; Ay 13:7-8 Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu,
au kumnyima haki asiye na hatia.
6 # Mit 10:14 Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi
na kinywa chake hualika kipigo.
7 # Za 140:9; 64:8; Mhu 10:12 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake
na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.
8 # Mit 26:22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;
huingia sehemu za ndani sana za mtu.
9 # Mit 28:24 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake
ni ndugu na yule anayeharibu.
10 # 2Sam 22:3; Za 61:3; 18:2 Jina la Bwana ni ngome imara,
wenye haki huikimbilia na kuwa salama.
11 # Mit 10:15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.
12 # Mit 11:2; 15:33 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,
bali unyenyekevu hutangulia heshima.
13 # Mit 20:25; Yn 7:51 Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza,
huo ni upumbavu wake na aibu yake.
14 # Mit 15:13; 17:22 Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa
bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?
15 # Mit 15:14; Efe 1:17 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa,
masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.
16 # Mwa 32:20; 39:2-6; 41:38-44; 1Sam 10:4 Zawadi humfungulia njia mtoaji,
nayo humleta mbele ya wakuu.
17Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi,
hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali.
18Kupiga kura hukomesha mashindano
na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana.
19 # 1Sam 17:28 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika
kuliko mji uliozungushiwa ngome,
nayo mabishano ni kama malango
ya ngome yenye makomeo.
20 # Mit 12:14 Tumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake,
atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake.
21 # Mit 13:2-3; Mt 12:37 Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi,
nao waupendao watakula matunda yake.
22 # Mit 12:4; 31:10; Ay 33:26 Apataye mke apata kitu chema
naye ajipatia kibali kwa Bwana.
23 # Mwa 42:13-16; Yak 2:3 Mtu maskini huomba kuhurumiwa
bali tajiri hujibu kwa ukali.
24 # 1Sam 20:42; Yn 15:13-15 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,
bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu