Mithali 25
NMM

Mithali 25

25
Mithali Zaidi Za Sulemani
1 # 1Fal 4:32 Hizi ni mithali zaidi za Sulemani, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:
2 # Kum 29:29; Rum 11:33; Mit 10:10-15 Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo,
bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.
3Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini,
ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.
4 # 2Tim 2:21 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha,
nako ndani yake kutatokea chombo
cha mfua fedha.
5 # 2Sam 7:13; Mit 20:8; 29:14 Ondoa waovu mbele ya mfalme,
nacho kiti chake cha enzi
kitaimarishwa kwa njia ya haki.
6Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme,
wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;
7 # Lk 14:7-10 ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,”
kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu.
Kile ulichokiona kwa macho yako
8 # Mit 17:14; Mt 5:25-26 usiharakishe kukipeleka mahakamani,
maana utafanya nini mwishoni
kama jirani yako atakuaibisha?
9 # Mt 5:25; 18:15 Kama ukifanya shauri na jirani yako,
usisaliti siri ya mtu mwingine,
10ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha
na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.
11 # Mit 15:23; Isa 50:4 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao
ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu
yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.
12 # Za 141:5; Mit 15:31 Kama vile kipuli cha dhahabu
au pambo la dhahabu safi,
ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima
kwa sikio lisikilizalo.
13 # Mit 13:17; Mit 10:26 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno
ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao,
huburudisha roho za bwana zake.
14 # Mit 20:6; Yud 1:12 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua
ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.
15 # Mhu 10:4; Mit 15:1; Mwa 32:4; 1Sam 25:24 Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa,
nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.
16 # Mit 25:27 Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha,
ukila zaidi, utatapika.
17Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache,
ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.
18 # Za 57:4; Mit 12:18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali
ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.
19 # Ay 6:14-20; 2Tim 4:16 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa,
ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.
20 # Dan 6:18; Rum 12:15 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi,
au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi,
ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.
21 # Kut 23:4; Mt 5:44; Rum 12:20 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale;
kama ana kiu, mpe maji anywe.
22 # 2Sam 16:22; Mt 5:44; Za 18:8 Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake,
naye Bwana atakupa thawabu.
23 # Ay 37:22; Za 105:5 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua,
ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.
24 # Mit 19:13; 21:9, 19 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,
kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
25Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka
ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.
26 # Mik 7:8 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au
kisima kilichotiwa taka
ndivyo alivyo mtu mwenye haki
akishiriki na waovu.
27 # Mit 27:2; Mt 23:12; Lk 14:11 Si vyema kula asali nyingi sana,
wala si heshima
kujitafutia heshima yako mwenyewe.
28 # Mit 16:32 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka
ndivyo alivyo mtu
ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu