Mithali 27
NMM

Mithali 27

27
1 # Lk 12:19-20; Yak 4:13; Mt 6:34; 1Fal 20:11 Usijisifu kwa ajili ya kesho,
kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.
2 # Mit 25:27 Mwache mwingine akusifu,
wala si kinywa chako mwenyewe;
mtu mwingine afanye hivyo
na si midomo yako mwenyewe.
3 # Ay 6:3; Es 1:12 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,
lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili.
4 # 1Yn 3:12 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,
lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?
5 # Gal 2:14 Afadhali karipio la wazi
kuliko upendo uliofichika.
6 # Za 141:5; Mit 28:23 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,
bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.
7 # Ay 6:7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,
bali kwa mwenye njaa
hata kile kilicho kichungu
kwake ni kitamu.
8 # Isa 16:2; Ay 39:14 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,
ndivyo alivyo mtu atangatangaye
mbali na nyumbani mwake.
9 # Es 2:12; Za 45:8 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,
nao uzuri wa rafiki huchipuka
kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.
10 # Mit 17:17 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,
tena usiende nyumbani mwa ndugu yako
wakati umepatwa na maafa.
Bora jirani wa karibu
kuliko ndugu aliye mbali.
11 # Mit 10:1; 23:15-16; Mwa 24:60 Mwanangu, uwe na hekima,
nawe ulete furaha moyoni mwangu,
ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote
anitendaye kwa dharau.
12 # Mit 22:3 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,
bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.
13 # Mit 20:16 Chukua vazi la yule awekaye dhamana
kwa ajili ya mgeni;
lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo
kwa ajili ya mwanamke mpotovu.
14 # Za 12:2 Kama mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu
asubuhi na mapema,
itahesabiwa kama ni laana.
15 # Es 1:18; Mit 19:13 Mke mgomvi ni kama
matone yasiyokoma ya siku ya mvua.
16Kumzuia yeye ni kama kuuzuia upepo
au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.
17Kama vile chuma kinoavyo chuma,
ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.
18 # 1Kor 9:7; Lk 19:12-27; Kum 20:6 Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake,
naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.
19Kama uso uonekanavyo kwenye maji,
ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonyesha alivyo.
20 # Mit 30:15-16; Hab 2:5; Mhu 6:7 Kuzimu na Uharibifu havishibi
kadhalika macho ya mwanadamu.
21 # Mit 17:3 Kalibu ni kwa ajili ya fedha
na tanuru kwa ajili ya dhahabu,
bali mtu hupimwa kwa sifa azipokeazo.
22 # Isa 1:5; Yer 5:3; Mit 23:35 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,
ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,
hutauondoa upumbavu wake.
23 # Mit 12:10; Yer 5:3 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako
ya kondoo na mbuzi,
angalia kwa bidii ng’ombe zako.
24 # Mit 23:5 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,
nayo taji haidumu vizazi vyote.
25 # Za 104:14 Wakati majani makavu yameondolewa
na mapya yamechipua,
nayo majani toka milimani yamekusanywa,
26wana-kondoo watakupatia mavazi
na mbuzi thamani ya shamba.
27Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi
kukulisha wewe na jamaa yako,
na kuwalisha watumishi wako wa kike.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu