Zaburi Utangulizi
NMM

Zaburi Utangulizi

Utangulizi
Kitabu hiki kinachopendwa sana leo hii kilikuwa pia kinapendwa zamani hizo. Ndani yake mnapatikana njia mbali mbali ambapo waumini kwa karne kadhaa walihusiana na Mwenyezi Mungu. Kila aina ya hisia ya mwanadamu yaweza kuwasilishwa mbele za Mwenyezi Mungu ili aibariki. Kuna huzuni na furaha, hasira na utulivu, shaka na imani, toba na sifa. Kuna kumbukumbu ya mambo yaliyopita, mgongano wa shida za wakati huu maishani, na maono ya siku za kesho zilizojaa utukufu. Katika maeneo kadhaa, Masiya wa Mungu, Isa Al-Masihi, anaonyeshwa katika mateso na utukufu wake.
Kitabu cha Zaburi kilitumiwa kama vile vitabu vya nyimbo vinavyotumiwa leo hii, katika ibada za hadharani na za mtu binafsi.
Wazo Kuu
Kimsingi kitabu cha Zaburi kinafunza kwamba Mwenyezi Mungu anashughulikia mahitaji ya watu wake kibinafsi, na kwamba anataka tuje kwake jinsi tulivyo tu. Hatuhitaji kusuluhisha shida zetu kabla ya kumwendea; tunamwendea kwa suluhisho. Kila mahali tulipo, haijalishi jinsi tunavyojisikia na lile tumefanya: ikiwa tutajitoa kwa Mwenyezi Mungu, yeye yuko tayari kutusaidia na kutupa nguvu za kuishi tena. Uongozi na utawala wa Mwenyezi Mungu kwa vitu vyote pia unaonekana. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu anatawala kila kitu, anaweza kutusaidia tunapomgeukia kwa ukombozi.
Mwandishi
Mwandishi mkuu ni Daudi, na pia wengine wengi.
Tarehe
Karne ya 10 K.K. na baadaye.
Mgawanyo
• Kitabu cha kwanza cha Zaburi 1–41
• Kitabu cha pili cha Zaburi 42–72
• Kitabu cha tatu cha Zaburi 73–89
• Kitabu cha nne cha Zaburi 90–106
• Kitabu cha tano cha Zaburi 107–150.

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu