Ufunuo Utangulizi
NMM

Ufunuo Utangulizi

Utangulizi
Kitabu hiki kisichoeleweka rahisi kina sehemu mbili, sehemu ya kwanza ikiwa ni barua kwa makanisa saba katika Asia Ndogo (1–3), na ya pili ikiwa ni mfululizo wa maono yanayohusu maisha na mateso ya watu wa Mwenyezi Mungu, kushindwa kwa uovu, kurudi kwa Al-Masihi, hukumu ya mwisho, utawala wa miaka elfu moja duniani, na hali ya mbinguni (4–22). Sehemu kubwa ya maono hayo inaelezea mfululizo wa adhabu kali inayomwagiwa ulimwengu (yaani lakiri, tarumbeta na mabakuli) ambapo gadhabu ya Mwana-kondoo wa Mungu (Isa) inaonyeshwa. Ndani ya mkusanyiko wa maono haya ni maono ya mateso ya watu wa Mwenyezi Mungu waliofia imani wakiwa mbinguni na wateule wanaoteswa duniani. Maono haya yanaendelea mbele na kufikia kikomo kwa makabiliano kati ya Kahaba na Babeli (wakisimamia Uovu) na ushindi wa Neno la Mwenyezi Mungu, ambaye ni Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana (19:16), anayekuja kuuangamiza uovu na kuandaa karamu kwa waumini: “Amen! Njoo, Bwana Isa” (22:20).
Wazo Kuu
Kitabu hiki cha kusisimua kinaonyesha Al-Masihi ambaye wakati mmoja aliaibishwa, aliye Mwana-kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, akitawala dunia katika nyakati za mwisho, na pia akileta wema wa milele kwa kuangamiza uovu na kusimamisha haki milele na milele. Ni tumaini dhahiri la Mkristo kwamba wakati mmoja mambo yote yatakuwa mema, naye Mwenyezi Mungu atakuwa yote ndani ya yote. Machozi yatafutwa, nazo kifo, majonzi, kilio, na uchungu zitaondolewa milele (21:4). Ujumbe huu wa kutia moyo ni wa waumini wote wa wakati wote.
Mwandishi
Mtume Yohana.
Mahali
Kisiwa cha Patmo.
Tarehe
Kama 90-96 B.K.
Mgawanyo
• Maono ya kufungua (1:1-20)
• Barua saba kwa Makanisa saba (2:1–3:22)
• Maono kuhusu Mwenyezi Mungu na Mwana-Kondoo (4:1–5:14)
• Lakiri saba za hukumu (6:1–8:5)
• Tarumbeta saba za hukumu (8:6–11:19)
• Maono kuhusu vita ya duniani na mbinguni (12:1–14:20)
• Mabakuli saba ya hukumu (15:1–16:21)
• Hukumu juu ya Kahaba Babeli (17:1–19:21)
• Mwisho wa dunia, na wakati ujao (20:1–22:21).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu