Utangulizi
Paulo alikuwa Korintho katika safari yake ya tatu ya kueneza Injili, na alikuwa anapanga kwenda Rumi, lakini hakuwa amefika huko hapo awali. Barua hii iliandikwa kwa kusudi lake kujijulisha kwa kanisa, na pia kutoa muhtasari wa mafunzo yake ya imani. Kwa sababu ya lengo hili la mwisho, ndiyo barua iliyoandikwa kwa mpangilio wa kipekee katika barua zote za Paulo. Anaanza kwa kuonyesha hali ya dhambi ya mwanadamu yeyote. Siyo Myunani wala Myahudi aliye na haki kisheria ya kusimama mbele za Mwenyezi Mungu kwa kuwa dhambi imeondoa uhalali wowote. Lakini Mwenyezi Mungu kupitia neema yake aliingilia kati, wakati bado tukiwa wenye dhambi, na akafungua njia ya sisi kupatana naye (5:8). Kutoka kwa jambo hili twaweza kupata maisha ya ushindi ya Ukristo. Paulo baadaye anajadili swala la sehemu ya Wayahudi katika mpango wa Mwenyezi Mungu (9–11), akimalizia na mfululizo wa maagizo yanayohusu maadili mema.
Wazo Kuu
Haki ya Mwenyezi Mungu, hali yake kushirikiana na ulimwengu kwa haki, na mpango wa haki wa wokovu ni mambo yanayosisitizwa katika kitabu hiki. Mwenyezi Mungu anaonyeshwa kuwa Mungu mkuu na mtakatifu wa ulimwengu ambaye hawezi kuzilegeza sheria zake kwa maana zina msingi katika asili yake. Lakini kupitia sheria hizo, aliweka mpango wa wokovu kwa Wayahudi na Wayunani pamoja kwa kumtuma Mwanawe kutoka mbinguni kuja kufia dhambi za ulimwengu. Sasa yeyote anayemwamini Isa ataokolewa (10:9), na kupewa nguvu za Mwenyezi Mungu za kushinda dhambi maishani mwake. Hakuna chochote chaweza kumtenganisha muumini kutoka kwa Mwenyezi Mungu na upendo wake (8:38, 39).
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Korintho.
Tarehe
Kama mwaka wa 58 au 59 B.K.
Mgawanyo
• Utangulizi (1:1-17)
• Dhambi, na wokovu kwa imani katika Al-Masihi (1:18–5:21)
• Ushindi dhidi ya dhambi kupitia nguvu za Al-Masihi (6:1–8:39)
• Mpango wa Mwenyezi Mungu kwa Wayahudi (9:1–11:36)
• Kanuni za kuishi maisha ya Kikristo (12:1–15:13)
• Maneno ya mwisho (15:14–16:27).