Utangulizi
Paulo alimwandikia mshiriki wake Tito waraka huu muda mfupi tu baada ya kumwachia wajibu wa kuliangalia na kuliimarisha kanisa katika kisiwa cha Krete. Wajibu wa Tito ulikuwa kuwateua wazee wa kanisa, kuwaweka wakfu, na kuwafundisha kushika misingi ya imani ya Kikristo. Ilimbidi Paulo aeleze kwa kina kuhusu sifa za wazee wa kanisa, na pia kutoa maagizo kwa waumini. Paulo aligusia matatizo yanayowapata watumishi wa Mwenyezi Mungu, na jinsi matatizo haya yanavyoweza kutatuliwa.
Wazo Kuu
Paulo katika barua hii anakazia kuhusu kuishi maisha yanayofaa ya Kikristo katikati ya uovu ulioko duniani. Ingawa katika maisha yetu hapa duniani tumezungukwa na uovu na chuki, hatuna budi kuonyesha maishani mwetu mazao ya neema ya Mwenyezi Mungu. Maisha kama haya yataleta mabadiliko wakati ambapo maneno pekee hayana matokeo.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Hapajulikani.
Tarehe
65 B.K.
Mgawanyo
• Salamu binafsi (1:1-4)
• Kuhusu kutiwa wakfu kwa wazee wa kanisa (1:5-16)
• Maelezo ya jumla kuhusu waumini (2:1-15)
• Maagizo kuhusu maisha yawapasayo Wakristo (3:1-15).