UTANGULIZI
Kitabu hiki ni mojawapo ya vitabu vya Biblia vinavyojulikana kama “Vitabu vya Deuterokanoni” vitabu ambavyo havimo katika orodha ya vitabu vya Biblia katika Biblia ya Kiebrania. Biblia ya Septuajinta (LXX) inaorodhesha kitabu hiki kati ya kitabu cha Yeremia na kitabu cha Maombolezo. Katika kitabu hiki, sura ya sita inajulikana kama Barua ya Yeremia. Katika LXX, kitabu cha Maombolezo kimetenganisha Barua ya Yeremia na kitabu cha Baruku, lakini Biblia ya Vulgata inaweka Barua hiyo pamoja na kitabu cha Baruku kama sura ya 6.
Kitabu hiki kina jina la katibu wa nabii Yeremia (taz Yeremia 45:1). Walakini kitabu chenyewe hakina uhusiano wa mambo na huyo nabii. Mitindo ya utungaji inayoonekana sehemu mbalimbali inadhihirisha kwamba labda mtu mwingine au watu wengine walihusika kama waandishi.
Mtindo wa maandishi ya kitabu cha Baruku
Kitabu hiki kinajumuishwa pamoja na vitabu vya maandishi ya hekima. Kitovu chake ni sheria ambayo inachukuliwa kama njia ya kufikia hekima. Wataalamu wa mambo ya Biblia wanabainisha sehemu nne katika kitabu hiki ambazo zinatofautiana kwa mtindo na mambo yaliyomo: Baada ya utangulizi unaoonesha shabaha ya kitabu na jinsi kinavyopaswa kuchukuliwa (1:1-14), tuna kitovu cha kitabu: Sala au maombi ambayo yanakiri hatia (kuungama dhambi) lakini pia pamoja na matumaini (1:15–3:8), kisha kuna utenzi wa hekima ambamo hekima inasemwa kuwa sawa na sheria (3:9–4:4); kisha panafuata sehemu ya kinabii ambamo nabii anawafariji watu kwa kuwakumbusha matumaini ya kimasiha (4:5–5:9). Sura ya 6 ya kitabu hiki ambayo inaitwa “Barua ya Yeremia” inahusu kufifia au kuzorota kwa ibada kwa Mungu. Aya hizo sabini na tatu za sura ya sita inayojulikana kama Barua ya Yeremia (taz pia Yer 29:1-23) ni hotuba kali dhidi ya kuabudu sanamu na kuamini miungu mingine (msingi wa kauli hiyo dhidi ya miungu ya uongo Yer 10:11). Mara kwa mara barua inarudiarudia maneno muhimu: Sanamu si miungu wala miungu haiwezi kuchanganywa na yule aliye Mungu wa kweli.