Esta UTANGULIZI
SCLDC10

Esta UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu hiki kina mhusika mkuu ambaye ni mwanamke mmoja wa Kiyahudi aitwaye Esta ambaye aliolewa na mfalme wa Persia. Kitabu chenyewe, kama vile kitabu cha Ruthu, Yudithi na Tobiti ni simulizi. Lengo la simulizi hilo, kama inavyodhihirishwa katika sura ya 9:20-32, ni kuonesha chanzo na umuhimu wa sikukuu moja ya Wayahudi iitwayo Purimu. Katika sikukuu hiyo, Wayahudi walisherehekea kuokolewa kwao kutoka tishio kubwa la kuangamizwa.
Kitabu hiki cha Esta kina muundo wa aina mbili: Muundo wa kwanza, mfupi zaidi, ni ule wa Biblia ya Kiebrania; muundo wa pili, mrefu zaidi, ni ule wa Biblia ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX). Sehemu zifuatazo za Biblia ya Kigiriki hazimo katika Biblia ya Kiebrania: Ndoto ya Mordekai (A 1-11) na maelezo yake (F 1-10) maagizo mawili ya mfalme Ahasuero (B 1-15 na E 1-16); sala ya Mordekai (C 1-11); sala ya Esta (C 12-19); Esta anamwendea mfalme mara ya pili (D 1-26). Sehemu hizo zote zimechapwa kwa mwandiko wa italiki.
Muundo huo wa Biblia ya Kigiriki, tofauti na ule wa Biblia ya Kiebrania, unaonesha wazi zaidi kuhusika kwake Mungu katika kuongoza historia na mambo ya taifa lake, hali katika Esta makala ya Kiebrania Mungu hatajwi waziwazi ingawa katika 4:14 panagusia kuhusika kwake Mungu katika kuwaokoa watu (ikiwa neno mbinguni linaleweka kwamba linatumika kumtaja Mungu mwenyewe). Hata hivyo, kuna tofauti kadha wa kadha kati ya makala ya Kigiriki na ile ya Kiebrania kiasi cha kutatanisha: Kadiri ya A:3 Mordekai ndiye anayemwarifu mfalme juu ya mpango wa siri wa kumwumiza na anapewa tuzo mara. Lakini katika 2:22 Esta ndiye anayemwarifu mfalme kwa niaba ya Mordekai, naye Mordekai hapewi tuzo ila mpaka tu baadaye (6:11). Katika A:17 Hamani alimchukia Mordekai kwa kuwa yeye aliwashtaki wale waliopanga kumdhuru mfalme; lakini katika Kiebrania (3:5) ni kwa sababu Mordekai alikataa kumwinamia Hamani kwa heshima. Tatizo kati ya makala ya Kigiriki na ile ya Kiebrania ya kitabu hiki cha Esta ni la kudumu, walau mpaka sasa.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  

Learn More About BIBLIA Yenye Vitabu vya Deuterokanoni HABARI NJEMA