Tobiti UTANGULIZI
SCLDC10

Tobiti UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu cha Tobiti ni simulizi la kisa cha jamaa moja. Palikuwa na mtu mmoja huko Ninewi jina lake Tobiti. Yeye (wa kabila la Naftali) alikuwa amepelekwa uhamishoni huko. Alikuwa mtu aliyeshika sheria, aliyewasaidia maskini lakini akapata balaa la kuwa kipofu. Na huko Ekbatana aliishi na jamaa yake Tobiti, jina lake Ragueli. Huyo alikuwa na binti yake aitwaye Sara. Sara naye alikuwa na balaa: Wanaume saba walimwoa lakini kila mmoja kabla ya kujamiiana naye usiku wa harusi aliuawa na jini moja liitwalo Asmodeo. Basi Tobiti na Sara kila mmoja kwa maombi yake wanamlilia Mungu kuhusu mikasa yao angalau wafe. Lakini Mungu anayasikiliza maombi yao jinsi apendavyo mwenyewe. Anamtuma malaika wake Rafaeli (jina lenyewe lamaanisha “Aponyaye ni Mungu”) ambaye anamsindikiza Tobia salama mpaka kwa Ragueli, anamsaidia hata akamwoa Sara na kulifukuza lile jini, anamrudisha kwa baba yake na kumponya.
Simulizi hili ni la kufundisha na katika fundisho hilo mkazo upo katika kusaidia maskini na wajibu wetu juu ya wafu; vilevile simulizi lenyewe laonesha mfano mwema wa maisha ya jamaa. Zaidi ya hayo yote wema wa Mungu wadhihirishwa katika matendo ya malaika Rafaeli ambaye ni mjumbe maalumu wa Mungu na kutuonesha kwamba wema wake na uangalizi wake upo pamoja nasi kila siku.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  

Learn More About BIBLIA Yenye Vitabu vya Deuterokanoni HABARI NJEMA