UTANGULIZI
Kitabu cha pili cha Wamakabayo kinasimulia kwa jumla habari zile zile zinazosimuliwa na kitabu cha kwanza cha Wamakabayo katika sura zake 1-7. Kinaanza na mfalme Seleuko wa Nne, aliyetangulia Antioko Epifani na kuishia na habari za kumshinda Nikano wakati Yuda Makabayo alipokaribia kufa.
Utungaji wa vitabu hivi viwili ni tofauti sana. Mtungaji wa kitabu cha pili amekiandika kitabu chake katika lugha ya Kigiriki. Habari zake ni muhtasari wa vitabu vitano vilivyoandikwa na Yasoni mtu fulani wa Kirene (2:23). Mtungaji anakusudia kuwafurahisha na kuwafundisha wasomaji wake (2:25; 15:39). Ushindi umepatikana kwa uongozi wa Yuda Makabayo aliyesaidiwa na matukio ya mbinguni. Yote ni kazi ya fadhili za Bwana (2:19-22). Hata madhulumu yenyewe ni huruma za Mungu kwa vile Mungu anasahihisha makosa ya taifa hilo kabla ya kufikia kikomo cha uovu wake (6:12-17).
Kitabu kimeandikwa kwa ajili ya Wayahudi wa Iskanderia, mji mkuu wa Misri. Mtungaji anajaribu kuamsha mioyo yao wajiunge zaidi na Wayahudi wa Yerusalemu. Ana shabaha ya kuwavuta wajishughulishe zaidi na hekalu la Yerusalemu na Torati. Taratibu ya kitabu inalenga shabaha hiyo.
Baada ya kusimulia habari za Heliodoro zinazoonesha utakatifu wa hekalu usioweza kuvunjika (3:1-40) zinafuata habari za kifo cha mdhalimu Antioko Epifani, aliyelinajisi hekalu. Sehemu ya kwanza inakoma kwa kuingiza sikukuu ya kutabaruku hekalu (4:1–10:8). Sehemu ya pili (10:9–15:36) inakwisha hivi hivi na habari za kifo cha mdhalimu Nikano aliyehatarisha hekalu. Inamalizika pia kwa kuweka sikukuu ya kumbukumbu ya kumshinda Nikano. Katika barua za mwanzoni (1:1–2:18) Wayahudi wa Yerusalemu wanawaalika Wayahudi wa Misri waadhimishe pamoja nao sikukuu ya kutabaruku hekalu.
Tukilinganisha vitabu hivi viwili tunaona pengine tofauti hata katika kusimulia mambo yale yale. Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba kitabu cha kwanza kinasimulia habari za historia kikamilifu zaidi kuliko kitabu cha pili. Tofauti zilizoko zinafahamika tu ikiwa tunakumbuka shabaha mbalimbali za watungaji. Mtungaji wa kitabu cha kwanza anakusudia kubainisha kama Mungu aliwasaidia Wayahudi katika matukio ya kihistoria. Kwa hiyo anaona lazima kisimulie habari sawasawa. Kumbe kitabu cha pili kinataka kufurahisha watu na kuwavuta Wayahudi wa Misri ili washirikiane zaidi na Wayahudi wa Yerusalemu. Kupata shabaha hiyo anatoa muhtasari wa vitabu vya Yasoni wa Kirene bila kuhakikisha ukweli wa habari za Yasoni. Hivyo hakusudii kufuata sheria za utaalamu wa historia juu ya habari anazozisimulia.
Kitabu cha pili ni cha maana sana kwa sababu ya mafundisho yake ya kidini. Kinafundisha wazi ufufuo (7:9), malipo baada ya kufa (12:41-46), stahili za mashahidi (6:18–7:41), sala za watakatifu kwa ajili yetu (15:12-16).
Kitabu hiki kimeandikwa baada ya mwaka 124 K.K. ulio tarehe ya barua ya kwanza (1:9).