Esta (Gir) 1
RSUVDC

Esta (Gir) 1

1
Mfalme Ahasuero Amfukuza Malkia Vashti
18 #Ezr 4:6 Katika nyakati za Ahasuero; Ahasuero aliyetawala mikoa mia moja na ishirini na saba, kutoka India mpaka Kushi;#1:1 au Ethiopia. 19 siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Susa, mji mkuu ngomeni; 20 mwaka wa tatu wa kutawala kwake, aliwafanyia karamu wakuu na mawaziri wake; wakuu wa majeshi ya Uajemi na Umedi; watu maarufu na wakuu wa mikoa, wakihudhuria mbele zake. 21 Akawaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, yaani siku mia moja na themanini. 22 Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Susa mji mkuu, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika ukumbi wa bustani ya ngome ya mfalme. 23 Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawati, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu yenye nakshi ya vito vyekundu, marumaru, lulu za manjano na nyeusi na mawe ya thamani. 24 Wakawanywesha kileo katika vyombo mbalimbali vya dhahabu, na divai tele ya kifalme, kufuatana na ukarimu wa ufalme; 25 Walikunywa kama ilivyoamriwa, bila kushurutishwa; maana mfalme aliwaagiza watumishi wahudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. 26 Naye Vashti, malkia, akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero.
27 Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake, 28 wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. 29 Bali Vashti, malkia, hakutii amri ya mfalme, alikataa kuja kama alivyoamriwa na mfalme kupitia kwa matowashi; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. 30 Basi mfalme akawaambia wenye hekima, waliojua sheria;#1:13 au walio na elimu ya nyakati. maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; 31 na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale wakuu saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, 32 Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba?
33 Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na wakuu wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. 34 Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. 35 Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliozisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maofisa wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele. 36 Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. 37 Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo. 38 Basi neno hili likawapendeza mfalme na wakuu wake; naye mfalme akafanya kama alivyopendekeza Memukani. 39 Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI