2
Esta Afanywa malkia
1 Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake. 2 Basi watumishi wa mfalme waliomhudumia walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri; 3 naye mfalme aweke wasimamizi katika mikoa yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Susa, mji mkuu kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi wa nyumba ya mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso. 4 Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo.
5 Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Susa, mji mkuu; jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, wa kabila la Benyamini; 6 #2 Fal 24:10-16; 2 Nya 36:10,20 ambaye alikuwa amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadreza,#2:6 Au, Nebukadneza. mfalme wa Babeli, alimchukua. 7 Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo zuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake. 8 Basi amri ya mfalme na mbiu yake iliposikiwa, wasichana wengi wakakusanyika huko Susa, mji mkuu mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. 9 Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na chakula chake, na vijakazi saba wa nyumbani mwa mfalme ili wamhudumie. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. 10 Naye Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. 11 Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na yale yatakayompata.
12 Basi zamu ya kila mwanamwali kuingia kwa mfalme Ahasuero, iliwadia baada ya kutayarishwa kulingana na sheria ya wanawake kwa miezi kumi na miwili; kwa kuwa ndivyo zilivyotimia siku zao za utakaso, miezi sita kwa mafuta ya manemane, na miezi sita kwa manukato na vifaa vya utakaso wa wanawake; 13 mwanamwali huingia hivyo kwa mfalme; kila alichotaka alipewa kwenda nacho kutoka katika nyumba ya wanawake ili kuingia katika nyumba ya mfalme. 14 Huenda jioni, na asubuhi hurudi katika nyumba ya pili ya wanawake, mikononi mwa Shaashgazi, msimamizi wake mfalme, aliyewalinda masuria. Wala haingii tena kwa mfalme, isipokuwa awe amempendeza mfalme, naye akaitwa kwa jina. 15 Wakati ilipowadia zamu yake Esta, binti Abihaili, mjomba wake Mordekai, ambaye alimtwaa kuwa binti yake, ili aingie kwa mfalme, yeye hakutaka kitu, ila vile vilivyoagizwa na Hegai, msimamizi wake mfalme, aliyewalinda wanawake. Naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona. 16 Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kutawala kwake. 17 Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji la kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti.
18 Ndipo mfalme alipowafanyia karamu kubwa wakuu wake wote na watumishi wake, yaani, karamu yake Esta; akafanya msamaha#2:18 Au msamaha wa kodi au siku ya mapumziko. katika majimbo yote, akatoa zawadi kulingana na ukarimu wa mfalme.
Mordekai agundua njama langoni
19 Basi mabikira walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa akiketi#2:19 Au alikuwa ameajiriwa kama msimamizi. mlangoni pa mfalme. 20 Esta alikuwa hajadhihirisha jamaa yake wala kabila yake, kama vile Mordekai alivyomwagiza; kwa maana Esta alikuwa akiyashika maagizo ya Mordekai, vile vile kama wakati alipolelewa naye. 21 Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili kati ya matowashi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, waliolinda milango ya vyumba vya mfalme, walikasirika sana, wakataka kumwua mfalme Ahasuero. 22 Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai. 23 Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.