B
Barua ya mfalme
14 Hii ndiyo nakala ya barua: Mfalme mkuu Artashasta anayaandika maneno haya kwa wakuu wa majimbo mia moja ishirini na saba, toka Bara Hindi hadi Kushi, na kwa maofisa walio chini yao: 15 Kwa kuwa nimepata kutawala mataifa mengi na kuimiliki dunia yote – wala si kama ninaufurahia huo uwezo wangu kwa kiburi, ila nia yangu ni kuyaongoza maisha yangu kwa kiasi na upole – kwa hiyo nimetaka kuthibitisha maisha ya raia wangu katika utulivu wa daima, na kuufanya ufalme wangu uwe na amani, hata mtu apite salama toka mpaka hata mpaka, na kuirudisha ile hali ya amani inayotakiwa na watu wote. 16 Basi, nilipouliza kwa washauri wangu jinsi hali hiyo itakavyopatikana, Hamani, mwenye busara nyingi barazani petu, ambaye amesifiwa sana kwa nia njema aliyo nayo kwetu siku zote na kwa uaminifu wake usio badilika, kupandishwa awe mtu wa pili katika ufalme, 17 yeye ametuonesha ya kuwa miongoni mwa mataifa ya ulimwengu wametawanyika watu wa nia mbaya waliofarakana na mataifa yote mengine kwa sheria zao, ambao siku zote huzidharau amri za wafalme, hata umoja wa ufalme unaotakiwa nasi haupatikani. 18 Basi, kwa sababu tunafahamu ya kuwa taifa hili peke yake linapingana daima na watu wote, akifuata kwa ukaidi namna ya maisha isiyopatana na sheria, nakuitakia serikali yetu mabaya, wakijitahidi kuudhuru ufalme wetu kwa kila njia ili usipate kuthibitika – 19 kwa sababu hiyo tumetoa amri kama wale waliotajwa katika barua mtakazoandikiwa na Hamani, msimamizi wa mambo yetu na baba yetu wa pili, waangamizwe wote kwa upanga wa adui zao, pamoja na wake zao na watoto wao, bila huruma wala rehema, siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili, Adari, mwaka huu. 20 ili wale wenye nia mbaya, katika zamani zilizopita na sasa pia, washushwe kuzimu wote kwa siku moja, na hivyo wauache ufalme wetu ukae salama bila hofu ya adui.
21 Nakala ya andiko hilo ilitakiwa kutolewa katika kila mkoa, ili kuwaarifu watu wote wajiandae kwa ajili ya siku hiyo. 22 Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika.