Esta (Gir) C
RSUVDC

Esta (Gir) C

C
Sala ya Mordekai
18 Ndipo Mordekai alimsihi BWANA, akizikumbuka kazi zake BWANA, akasema: 19-20 Ee BWANA, BWANA, mfalme Mwenyezi; ulimwengu wote u katika uweza wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda kuwaokoa Israeli. 21-22 Maana Wewe umeviumba mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyopo chini ya mbingu, nawe ndiwe BWANA wa vyote wala hakuna awezaye kushindana nawe, BWANA. 23 Wewe unajua yote. Unajua ya kuwa si kwa jeuri, wala kwa kiburi, nilikataa kuinama mbele ya Hamani mwenye makuu. Hakika, kwa ajili ya wokovu wa Israeli ningekuwa tayari hata kuzibusu nyayo za miguu yake. 24 Ila nilifanya hayo nisitangulize utukufu wa binadamu mbele ya utukufu wa Mungu. Sitamsujudia yeyote ila Wewe, BWANA wangu, wala sikatai kwa kiburi. 25 Basi, sasa. Ee BWANA, Mungu, Mfalme, Mungu wa Abrahamu, uwaachilie watu wako; maana macho ya watu wanatuvizia ili kutuangamiza, nao wanatafuta kuuharibu urithi ambao umekuwa wako tangu milele. 26 Usilidharau fungu lako ulilojikombolea katika nchi ya Misri. 27 #Kut 3:6 h Yasikie maombi yangu uurehemu urithi wako, ugeuze matanga yetu yawe karamu, ili tuishi na kuliimbia jina lako, Ee BWANA; wala usiiharibu midomo yao wanaokuhimidi, Ee BWANA. 28 Na Israeli wote walilia sana, maana kufa kulikuwapo mbele ya macho yao.
Sala ya Esta
29-30 Malkia Esta naye alimkimbilia BWANA, akishikwa na uchungu wa mauti. Akazivua nguo zake za fahari akavaa nguo za huzuni na kilio, na badala ya manukato mazuri alijitia majivu na samadi kichwani; akajinyenyekeza mwili wake, hata mahali pa mapambo ya furaha alijifunika wa nywele zake zilizofumuliwa. Akamwomba BWANA wa Israeli, akisema: 31-32 BWANA wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mkononi mwangu. 33 Tangu nilipozaliwa katika kabila za jamaa yangu, nimesikia ya kuwa Wewe, BWANA, ulimchagua Israeli katika mataifa yote, na baba zetu katika jamaa zao, kuwa urithi wa daima, ukawatimilizia yote uliyoyaahidi. 34-35 Na sasa tumetenda dhambi mbele zako nawe umetutia mikononi mwa adui zetu, kwa sababu tumeitukuza miungu yao. Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki. 36-37 Wala haiwatoshi ya kuwa sisi tumo katika uchungu wa kufungwa, ila wamepeana mikono, wao na sanamu zao, kuondoa sheria iliyotoka kinywani mwako, na kuuharibu urithi wako, na kuziba midomo yao wanaokuhimidi, na kuuzimisha utukufu wa nyumba yako na madhabahu yako, 38 na kuvifumbua vinywa vya mataifa waisifu miungu ya uongo na kuwaadhimisha daima wafalme wa kibinadamu. 39 Ee BWANA, usiwape wasio miungu fimbo yako ya kifalme, wala wasitucheke katika maanguko yetu, bali uligeuze shauri lao juu yao wenyewe, na kuwaonya kwa adhabu yake yeye aliyetuanzia mambo hayo. 40 Utukumbuke, Ee BWANA; ujifunue wakati wa taabu yetu; unipe moyo thabiti, Ee Mfalme wa mbingu na BWANA wa milki zote. 41 #Ydt 9:13 s Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuza moyo wake apate kumchukia yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye. 42 Lakini utuokoe sisi kwa mkono wako; unisaidie mimi niliye peke yangu, bila msaidizi mwingine ila Wewe, BWANA. 43 Wewe unajua yote. Unajua ya kuwa naichukia fahari ya waovu, na kukikirihi kitanda chake asiyetahiriwa na cha kila mgeni. 44 Unajua ninavyolazimishwa, na jinsi ninavyoichukia ishara ya cheo changu iliyopo kichwani pangu siku ninazojionesha mbele ya watu. 45 #Dan 1:8; Ydt 12:2 Naichukia kama nguo iliyotiwa unajisi, wala siivai ninapokaa faraghani. Tena, mimi, mjakazi wako sijala mezani pa Hamani, wala kuhudhuria kwenye karamu yake, wala kunywa divai ya sadaka. 46 Mimi mjakazi wako sijajua furaha tangu siku niliyoletwa hapa hata sasa, ila katika Wewe, BWANA Mungu wa Abrahamu. 47 Ee Mungu, uweza wako ni juu ya yote; isikie sauti yao wasio na tumaini, utuokoe mikononi mwao wafanyao maovu, uniokoe katika hofu yangu.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI