Esta (Gir) E
RSUVDC

Esta (Gir) E

E
Tangazo la mfalme Artashasta
13 Haya ndiyo maneno ya barua: 14 Mfalme mkuu Artashasta kwa watawala wa nchi katika majimbo mia moja ishirini na saba toka Bara Hindi hata Kushi, na kwa wale wanaoupenda ufalme wetu, salamu. 15 Kuna wengine ambao wanapozidi kutukuzwa kwa ukarimu wa wafadhili huzidi kutakabari, hata, licha ya kujaribu kuwadhuru raia wetu tu, huanza kufanya mashauri juu ya wafadhili wao wenyewe, kwa sababu hawawezi kuzistahimili fadhili hizo nyingi. 16 Si kama huondoa shukrani miongoni mwa watu tu, ila pia huinuliwa kwa maneno makuu ya wapumbavu na kutumaini kuepukana na hukumu ya Mungu ajuaye yote anayeupatiliza uovu. 17 Hata mara nyingi wenye mamlaka wamedanganywa na maneno laini ya marafiki waliokabidhiwa kazi za utawala, na hivyo wameishiriki damu ya wasio na hatia na kutiwa katika maafa yasiyo na dawa, 18 kwa sababu watu hawa wameishawishi mioyo myema ya bwana zao isiyofikiri mabaya kwa hila ya maelekeo yao mabovu. 19 Basi, hayo niliyoyasema mtaweza kuona, si sana kwa kuzichungua taarifa za zamani, bali hasa kwa kuchunguza mambo ya siku hizi yaliyotendeka juzi juzi tu kwa uovu wao wasiostahili mamlaka waliyopewa. 20 Yatupasa kuangalia sana siku hizi zijazo tuufanye ufalme wetu uwe na utulivu na amani kwa watu wote. 21 si kwa kuyasikiliza maneno ya watu, ila kwa kuamua kwa haki na uangalifu mambo yanayoletwa mbele yetu. 22 Maana Hamani Mwana wa Hamedatho, Mmakedonia ni mgeni kabisa hana damu yoyote ya Kiajemi, na yeye hana kabisa dalili ya shukrani kwa wema wetu, huyo alikaribishwa akae kwetu, 23 akashirikishwa ule upendeleo tunaowaonesha watu wa mataifa yote, hata akaitwa baba yetu. Naye alipewa heshima na wote kwa kuwa alikuwa mtu wa pili baada ya mfalme mwenyewe. 24 Lakini yeye, kwa kuwa hakuweza kukistahimili cheo chake kikuu, alifanya shauri atunyang'anye ufalme wetu na uzima wetu, 25 na kwa ujanja na udanganyifu mwingi alijaribu kumwua, si Mordekai tu, aliye mwokozi wetu na mfadhili wetu wa daima, ila na Esta pia, mshiriki wa ufalme wetu, asiye na hatia, pamoja na taifa lao lote. 26 Maana kwa hila hizo alidhani kutuacha upweke pasipo msaidizi, hata awape Wamakedonia ufalme wa Waameji. 27 Nasi tumeona ya kuwa Wayahudi, ambao huyu mtu wa shari nyingi amewatoa wauawe, sio watenda maovu hata kidogo, bali hujitawala kwa sheria ya haki kabisa; 28 nao ni wana wake aliye Juu, Mwenyezi, Mungu aliye hai, atengenezaye mambo ya ufalme kwa ajili yetu na kwa ajili ya baba zetu kwa utaratibu bora kabisa. 29-30 Basi, afadhali msiyatimize yale yaliyoandikwa katika barua mlizoletewa na Hamani mwana wa Hamedatho, kwa sababu aliyeyatenda hayo ametundikwa penye mlango wa Susa pamoja na wote wa nyumba yake; Mungu anayetawala yote amemlipa upesi stahili zake. 31 Itangazeni nakala ya barua hii kila mahali; waacheni Wayahudi wazifuate sheria zao wenyewe, kawapeni silaha ili siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, Adari, siku ile ile, wapate kujilinda nao watakaowashambulia katika shida yao. 32 Maana Mungu anayetawala yote ameifanya siku hiyo kuwa siku ya furaha wala si ya kufa kwa taifa teule, 33-34 nanyi, basi, katika sikukuu zenu za ukumbusho, mtaiadhimisha kwa furaha kama siku maalumu, ili sasa na siku zote iwe siku ya wokovu kwetu na kwa Waajemi wenye nia njema, na ukumbusho wa maangamizo kwao wanaotuvizia. 35-36 Kwa hiyo mji wowote au nchi yoyote isiyoyafuata maagizo hayo itaharibiwa kabisa kwa upanga na kwa moto pasipo huruma, isipitiwe na mtu yeyote, bali ichukize daima hata kwa wanyama na ndege.
37 Nakala ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao. 38 Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Susa mjini.
39 Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawati na nyeupe, mwenye taji kubwa la dhahabu, na joho la kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Susa wakapaza sauti, wakashangilia. 40 Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. 41 Na katika kila mkoa, na kila mji, popote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, maana waliwaogopa Wayahudi.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI