UTANGULIZI
Esta ni mwanamke Myahudi ambaye alikuwa Malkia wa Uajemi na alihusika katika mpango mahsusi wa kuwaokoa Wayahudi wasiangamizwe (2:5-18). Esta ambaye alikuwa yatima alilelewa na ami wake Mordekai wa kabila la Benyamini. Mordekai alichukuliwa uhamishoni Babeli na baadaye akaishi Susa mji mkuu wa dola ya Uajemi.
Mwandishi wa Kitabu hiki anasimulia habari zilizomo kitabuni kwa uangalifu mwingi. Anaeleza hali na tabia ya mfalme Ahasuero, mke wake mfalme na jinsi Esta alivyopata kuwa malkia wa Uajemi.
Shabaha ya masimulizi haya ni kueleza jinsi watu wa Mungu walivyoshika imani yao wakiwa katika nchi ya kigeni. Vile vile simulizi la kitabu hicho, kwa namna moja au nyingine, kilikuwa na shabaha ya kuonesha asili na chanzo cha sikukuu ya Purimu ambayo iliadhimishwa kabla ya Pasaka.