Waamuzi UTANGULIZI
RSUVDC

Waamuzi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Baada ya Yoshua hakutokea mtu wa kurithi nafasi ya kuliongoza taifa la Israeli. Viongozi waliojitokeza walikuwa mashujaa walioongoza majeshi ya makabila yao katika vita vilivyokumba sehemu zao. Wakati wa amani viongozi hao walitawala sehemu zilizohusika na kila kabila lilishughlikia mambo yake. Viongozi hao wa kijeshi wanaitwa Waamuzi ambao huenda waliongoza makabila ya Waisraeli kwa kipindi cha miaka kama mia tatu na hamsini.
Kitabu hiki kinaitwa cha Waamuzi kwa kuwa masimulizi yake yanahusu viongozi wa kijeshi kumi na nane walioitwa jina hilo.
Katika Kitabu cha Waamuzi tunasimuliwa kuwa Waisraeli walipoingia katika nchi ya Ahadi hawakuiteka nchi hiyo yote mara moja. Sehemu fulani walishindwa kupaingia na nyingine walilazimika kukaa na makabila yaliyokuwa maadui zao. Aidha Waisraeli mara kwa mara walimuasi Mungu wakaiga desturi za dini za Wakanaani na kwa sababu ya uasi huo Mungu aliwaacha. Maadui walipohisi udhaifu wa kabila fulani la Waisraeli walilishambulia (3:1-8). Waisraeli walipotubu na kumlilia BWANA, Mungu aliwahurumia akamtuma kiongozi wa kijeshi aitwaye Mwamuzi, wakawashinda maadui akawaokoa (2:11-16; 3:9-15; 4:1-4; 6:1-10; 10:6-16; 31:1). Mungu aishiye milele ni wa upendo na huruma. Mwenye dhambi akitubu husamehewa. Ushindi wa Waisraeli haukutokana na uwezo wao bali uwezo wa Mungu. Kumtegemea Mungu, kutii Agano na maisha ya dini yao kuwa kitovu cha taifa ni mambo yaliyokosekana wakati huo hadi utawala wa kifalme ulipoanzishwa.
Yaliyomo:
1. Maelezo kuhusu ushindi wa Yoshua, Sura 1:1–2:10
2. Waamuzi wa Waisraeli, Sura 2:11–16:31
3. Machafuko katika Israeli, Sura 17–21

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI