Yudithi UTANGULIZI
RSUVDC

Yudithi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu cha Yudithi kinasimulia ushindi wa taifa teule juu ya maadui zake kwa ujasiri wa mwanamke fulani. Jemadari Holofene alitumwa na Nebukadreza mfalme wa Babeli, kujitwalia dunia yote na kuwashurutisha watu wa mataifa yote wamwabudu yeye Nebukadreza peke yake kama mungu.
Wayahudi wanakataa kumsujudia Nebukadreza. Wanajiwekea tayari jeshi dogo la kupigana na jeshi kubwa na la kutisha la Holofene. Wayahudi wamezungukwa na maadui katika mji wa Bethulia. Hawana maji tena. Kwa hiyo wako tayari kujitoa kwa Holofene. Katika hali hiyo ya hatari anajitokeza Yudithi mwanamke mjane mwenye busara na uchaji wa Mungu. Anawakaripia wakubwa wa Bethulia kwa kutokuwa na imani. Anamwomba Mungu amsaidie, anajiandaa kwa safari, anaondoka Bethulia na kujionesha mbele ya Holofene. Anatumia hila na ushawishi. Anapokuwa peke yake na jemadari aliyekwisha lewa anamkata kichwa. Askari wa Holofene wanapoona ya kuwa jemadari wao ameuawa wanashikwa na woga, wanatoroka. Wananchi wanamtukuza Yudithi na kwenda Yerusalemu, kumshukuru Mungu kwa shangwe.
Inaonekana kwamba mtungaji amekosa kwa makusudi katika kusimulia sawasawa habari za historia ya dunia. Anakusudia wasomaji wake wasishughulike mno na matukio yaonekanayo kwa macho ya mwili. Washughulike hasa na maana ya matukio hayo: Mungu na Shetani. Kitabu kinakusudia kubainisha ushindi wa Mungu juu ya Shetani kwenye nyakati za mwisho. Jemadari Holofene ni mfano wa enzi yote ya uovu. Yudithi, kama kiongozi wa taifa teule, ni mfano wa enzi yote ya wema.
Kundi la watu wanaosimama upande wa Mungu wanaonekana kuwa wanaangamizwa. Lakini Mungu anawapatia ushindi kwa mikono dhaifu ya mwanamke. Tena ushindi unapatikana kama tuzo kwa sala ya Yudithi na kushika kwake kwa uaminifu sheria ya usafi ya Torati. Kitabu kinatangaza wokovu, unaopatikana kwa wote walio na mapenzi mema wala si Wayahudi tu. Inaonekana kwamba mtungaji alichagua kwa makusudi Bethulia kama mji wa vita na wokovu. Bethulia kama mji wa wokovu mtungaji anadokeza kwamba Wasamaria watakombolewa pia. Tunafundishwa hayo pia katika habari za Akioro, Mkuu wa Waamoni, maadui wa Israeli. Inaonekana ya kwamba kitabu hiki kimetungwa katika Palestina kati ya miaka 120-80 K.K.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI