Nehemia UTANGULIZI
RSUVDC

Nehemia UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu hiki kimepewa jina la mtu aitwaye Nehemia (1:1) anayefikiriwa kuwa ndiye mwandishi wake. Nehemia ni Myahudi aliyekuwa uhamishoni, alipewa madaraka makubwa katika utawala wa Mfalme Artashasta wa Persia (1:11). Ijapokuwa alikuwa katikati ya watu wenye imani tofauti na yake, aliendelea kuwa mwaminifu na mtiifu kwa imani ya baba zake. Aliagizwa na Mfalme aende mjini Yerusalemu atawale na kurekebisha maisha ya wakazi wake kijamii, kisiasa na kiuchumi (1:1-2,10).
Kutokana na uaminifu wake alitekeleza aliyopaswa kufanya licha ya upinzani kutoka kwa maadui fulani. Wengi wa wakazi walimwunga mkono wakajenga kuta za Yerusalemu (2:11–7).
Nehemia alisimamia uwekaji wakfu wa kuta hizo (11:1–12:43). Baada ya mawaidha juu ya sheria ya BWANA yaliyotolewa na kuhani Ezra, Nehemia akiwepo, maisha ya kidini yalirekebishwa na watu wakayarudia tena maagano yao na Mungu (8:1–10:40; 12:44–13:31).
Kitabu cha Nehemia ni mfululizo wa vitabu vya Ezra na Mambo ya Nyakati kilichoandikwa kuonesha uaminifu na utiifu kwa Mungu, kwa agano lake, toba na katika kurekebisha maisha. Hapa Nehemia ameoneshwa kama mfano wa mtawala amchaye Mungu wake.
Yaliyomo:
1. Nehemia awaombea watu wake na kukubaliwa kwenda Yerusalemu, Sura 1–2
2. Ujenzi wa kuta za Yerusalemu, Sura 3–7
3. Sheria kusomwa, ungamo na ithibati, Sura 8–10
4. Ukuta wawekwa wakfu, Sura 11–12
5. Matengenezo ya maisha kidini, Sura 13

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI