Tobiti UTANGULIZI WA VITABU VYA TOBITI, YUDITHI NA ESTA
RSUVDC

Tobiti UTANGULIZI WA VITABU VYA TOBITI, YUDITHI NA ESTA

UTANGULIZI WA VITABU VYA TOBITI, YUDITHI NA ESTA
Vitabu vya Tobiti, Yudithi na Esta vina umoja fulani kwa sababu vitabu vyote vimetungwa kwa namna ile ile. Alama zao za pekee ni hizi:
1. Baadhi ya maneno ya vitabu hivi huhitilafiana sana katika nakala mbalimbali za zamani za kale, ambazo tunazo bado mpaka siku hizi. Kwa vitabu vya Tobiti na Yudithi tunazo tafsiri mbalimbali tu, na nakala zote za lugha ya asili zimepotea. Kwa kitabu cha Esta tunayo matoleo mawili, toleo moja fupi katika lugha ya Kiebrania, toleo refu katika lugha ya Kigiriki. Katika toleo la Biblia yetu maongezo ya tafsiri ya Kigiriki yamechapwa katika mshazari.
2. Wakristo wa karne za kwanza walitilia shaka kama vitabu hivyo ni kweli vitabu rasmi au sivyo. Waprotestanti hawakuzipokea sehemu zile zilizoandikwa kwa Kigiriki katika orodha yao ya vitabu rasmi.
3. Vitabu vyote vinaonekana kama mchanganyo wa matukio ya kweli na mambo yaliyobuniwa na watungaji wenyewe. Wanasimulia habari za historia ya dunia kwa uhuru mwingi. Kulingana na kitabu cha Tobiti, Tobiti baba-mtu alikuwa kijana wakati wa kifo cha Sulemani na kufarakana kwa makabila ya Israeli kwenye mwaka 931 Kabla ya Kristo Kuzaliwa (Tob 1:4). Tobiti alitekwa pamoja na kabila la Naftali mwaka 734 K.K. (Tob 1:10). Mtoto wake Tobia alifariki baada ya uangamizi wa Ninawi, mwaka 612 K.K. (Tob 14:15). Kadiri ya hesabu hizo Tobiti na Tobia wangalikuwa na umri mrefu wa ajabu. Katika kueleza jiografia wanasimulia pia mambo ya kustaajabisha. Hiyo ni baadhi tu ya mifano yenye masuala katika maelezo ya vitabu hivyo. Kwa sababu ya hali hiyo ya utungaji, ni vigumu kutofautisha kati ya mambo yaliyotukia kweli na mambo yaliyoongezwa na watungaji. Kutokana na tabia hiyo ya utungaji, nia na kusudi la watungaji hawa katika kuandika vitabu vyao inaonekana wazi. Walikusudia kutoa mafundisho ya dini, si kueleza historia ya dunia. Pia wanafundisha kweli za dini kwa kutoa mifano iliyo wazi.
KITABU CHA TOBITI
UTANGULIZI
Kitabu cha Tobiti kinasimulia habari za jamaa ya Tobiti. Tobiti amehamishwa mbali Ninawi. Ni mtu wa ibada na mkarimu tena mshika Torati hata kwenye makao yake mapya. Anageuka kuwa kipofu. Huko Ekbatana jamaa yake mmoja ana binti, jina lake Sara. Mara saba aliolewa, lakini mara saba usiku wa harusi mabwana zake mmoja baada ya mwengine waliuawa na jini lenye jina la Asmodeo. Sababu ya misiba hiyo Tobiti na Sara wanamwomba Mungu wapate kufa. Lakini Mungu anawasaidia wote wawili kupona na kuwageuzia huzuni yao iwe furaha. Anamtuma malaika wake Rafaeli, amsindikize mwana-mtu Tobia kwa Ragueli, baba ya Sara. Huko anamwoza Sara kwa Tobia na kumwonesha dawa ya kumponya baba yake kipofu.
Nia ya kusimulia habari hizi ni kuonesha kwamba Mungu huwatuza wale wanaoshughulikia marehemu na maskini. Kadhalika habari hizi ni mfano wa familia bora inayomtumikia Mungu na kuishi katika amani na upendo. Zaidi ya hayo inatufundisha ubora na heshima ya ndoa. Na juu ya hayo yote tunamwona Mungu anayeongoza mambo yote ya kila siku hapa duniani. Kitabu hiki kimeandikwa na Myahudi aliyeishi mbali na Palestina, labda huko Misri kati ya miaka 400-200 K.K.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 

Learn More About BIBLIA KISWAHILI